TUKIO kubwa linalosubiriwa na umma wa wapenzi wa soka Afrika hivi sasa ni mechi ya ufunguzi wa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) 2024, itakayochezwa leo Jumamosi, Agosti 2, 2025 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Tanzania.
Katika mechi hiyo itayochezwa kuanzia saa 2:00 usiku, timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ itakabiliana na Burkina Faso ‘Farasi Dume’ ambazo zipo katika kundi B la mashindano hayo ambalo pia linajumuisha timu za Jamhuri ya Afrika ya Kati, Mauritania na Madagascar.
Kitendo cha Mkoa wa Dar es Salaam kupata fursa ya kuwa na mechi za kundi B, mchezo mmoja wa robo fainali na mmoja wa nusu fainali ya fainali za CHAN ni jambo lililopokelewa kwa mikono miwili na Chama cha Mpira wa Miguu Dar es Salaam (DRFA) ambacho kinaona jambo hilo ni bahati kubwa na ya kipekee kwa mkoa huu.
Katika mahojiano maalum na gazeti hili, mwenyekiti wa DRFA ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Lameck Nyambaya anasema Dar es Salaam imepokea kwa mikono miwili fursa hiyo adhimu na itahakikisha mashindano hayo yanachezwa vyema.
“Niwe tu mkweli nimeridhika na maandalizi yanayofanyika kwa ajili ya CHAN 2024. Kwetu Mkoa wa Dar es Salaam hili ni jambo kubwa kwa vile linafanyika ndani ya mkoa wetu.
“Tumefurahia kuona tumepata fursa hii ya kuandaa tukio hili kubwa. Nasi kama mkoa tumejipanga kikamilifu kutoa sapoti yetu kwa serikali, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF),” anasema Nyambaya.

Nyambaya anasema mashabiki wa soka mkoani Dar es Salaam wanapaswa kuonyesha kwa vitendo wao ni vinara katika mpira wa miguu kwa kujitokeza kwa wingi uwanjani wakati wa fainali za CHAN hasa mechi ya ufunguzi.
“Haya ni mashindano makubwa ambayo yanafanyika hapa Tanzania kwa kushirikiana na Kenya na Uganda. Nitumie nafasi hii kualika mashabiki mbalimbali hasa wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi katika tukio la ufunguzi wa fainali za CHAN 2024, Agosti 2, 2025.
“Dar es Salaam ndiyo kitovu cha soka na ndiyo mkoa ambao una hamasa na msisimko mkubwa wa mpira wa miguu. Nina imani mashabiki watajitokeza kwa wingi katika tukio la ufunguzi ili kuendelea kuipa heshima Tanzania kama nchi ya kisoka,” anasema Nyambaya.
Nyambaya anasema DRFA ina imani kubwa namba ya mashabiki itakuwa kubwa viwanjani sio tu kwa mechi za Taifa Stars bali pia za timu nyingine zinazoshiriki CHAN.
Nyambaya kwa niaba ya DRFA anaipongeza na kuishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa sapoti kubwa hadi mashindano hayo yanafanyika.
“Napenda kumpongeza Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayofanya na kwa jinsi anavyotuunga mkono katika mpira wa miguu na hadi kuweza kuwashawishi viongozi wa CAF kutupa haya mashindano.
“Ni juhudi zake pia zimechangia CAF kuona ufunguzi wa haya mashindano unapaswa kufanyika hapa Dar es Salaam,” anasema Nyambaya.

Mashindano mengine marufuku
Katika kuhakikisha mawazo na hisia za mashabiki wa soka Dar es Salaam wanaelekeza katika fainali za CHAN, DRFA imetangaza kuzuia kwa muda mashindano mengine ya soka mkoani Dar.
“Watu waje kwa wingi tujaze uwanja. Tukijaza uwanja itasaidia timu ya Taifa kufanya vizuri. Naona timu imefanya maandalizi ya kutosha, TFF kwa kushirikiana na Serikali, timu imeweka kambi nje ya nchi ili kufanya maandalizi.
“Sisi kama DRFA tumechukua hatua, kwa kipindi hiki ambacho mashindano haya ya CHAN yatafanyika ni kuagiza vyama vyetu vya wilaya na washirika wengine kusimamisha au kusitisha mashindano mbalimbali katika mkoa wetu katika kipindi hiki.
“Kwa hiyo nisisitize tena mashindano yote katika mkoa wetu wa Dar es Salaam yatasimama katika kipindi chote cha mashindano ya CHAN hadi yamalizike ndipo yataendelea.
“Kwa kipindi hiki tuwe kitu kimoja, tuisapoti timu yetu ya Taifa na tuwapokee wageni wanaokuja nchini kwa ajili ya mashindano ya CHAN,” anasisitiza Nyambaya.
Mashabiki kuzoa tiketi 1000
Nyambaya anasema DRFA itatoa sapoti ya kugawa tiketi zaidi ya 1000 kwa mashabiki wa soka Dar es Salaam ili wapate fursa ya kwenda kutazama mechi ya ufunguzi wa mashindano hayo.
“Tumeandaa utaratibu wa kuwapatia mashabiki na tumeandaa tiketi za kutosha ambazo tunazipanga ziende kugawiwa kwa mashabiki na nimeona tupate tiketi angalau 1000 ili tuweze kuzigawa watu waweze kuishangilia timu yetu ya taifa.
“Shabiki ni mtu muhimu sana katika kusapoti timu yetu ya taifa. Sisi kama DRFA tumejiandaa vizuri katika kuhakikisha mashabiki wanajitokeza kwa wingi kuisapoti Taifa Stars, pia kutoa sapoti nyingine ndogondogo,” anasema Nyambaya.

Nyambaya anatoa wito kwa timu za Ligi Kuu zilizopo Dar es Salaam hasa Yanga na Simba kuungana kwa ajili ya kuhamasisha timu ya taifa.
“Timu ikifanya vizuri haitokuwa ya mtu bali ni ya taifa. Nichukue nafasi hii kumpongeza Ofisa Habari wetu wa TFF kushirikiana na wasemaji wa Simba na Yanga. Nitumie nafasi hii kuwaomba wasemaji wa klabu kushirikiana katika promosheni.
“Kila mmoja azungumze na mashabiki wake na atumie nafasi yake kuwaomba watu wajitokeze kwa wingi viwanjani kuisapoti timu ya taifa. Timu ikifanya vizuri, sifa tunapata kama nchi na sio mtu mmojammoja,” anasema Nyambaya.