MICHUANO ya Fainali za Ubingwa kwa Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) 2024 inaanza leo, Agosti 2, 2025 kwa mechi ya ufunguzi kati ya Tanzania (Taifa Stars) dhidi ya Burkina Faso itakaochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kuanza kwa michuano hiyo kunaifanya Stars mezani kuwa na kitita cha Sh9 bilioni kama zawadi endapo itatwaa ubingwa unaoshikiliwa na Senegal kwa sasa.
Hiyo inatokana na awali Rais Samia Suluhu Hassan kuahidi kutoa Sh1 bilioni endapo itabeba ubingwa wa mashindano hayo.
Ukiweka kando ahadi hiyo, pia fainali za mwaka huu zimevuka rekodi kwa kuongezeka kiwango cha zawadi za fedha zilizotangazwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), hali inayozifanya timu 19 shiriki ikiwemo Taifa Stars kuwa na hesabu kali za kuziwania.
Kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo mwaka 2009, mshindi wa CHAN 2024 ataondoka na dola 3.5 milioni (Sh8.9 bilioni za Kitanzania), ikiwa ni ongezeko la asilimia 75 kutoka mashindano yaliyopita ambapo Senegal ilikuwa bingwa na kubeba kitita cha Dola za Kimarekani milioni 2 (Sh5.1 bilioni za Kitanzania). Mbali na hilo, zawadi za jumla zimeongezeka kwa 32% hadi kufikia dola milioni 10.4 (Sh26.5 bilioni za Kitanzania).
Michuano ya mwaka huu inaendeshwa kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda, ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika ikiandaliwa na nchi tatu, pia ni mara ya kwanza kuchezwa Ukanda wa Afrika Mashariki.
Tofauti na mashindano ya nyuma, mwaka huu CAF pia imezindua kombe jipya lenye muundo wa kisasa, likiwa ni alama ya mwanzo mpya. Ubunifu wa kombe hilo unaakisi mwelekeo mpya wa CHAN michuano ya hadhi, mshikamano na maendeleo ya wachezaji wa ndani.
Kwa mujibu wa taarifa ya CAF, lengo la mabadiliko haya ni kuimarisha ushindani na kuwapa motisha zaidi wachezaji wa ndani, ambao mara nyingi wamekuwa na nafasi ndogo licha ya kuwa na vipaji vikubwa.
Hivyo basi, endapo Taifa Stars ikitwaa ubingwa, kwanza itavuna Sh8.9 bilioni kutoka CAF, sambamba na Sh1 bilioni ambazo ni ahadi ya Rais Samia na kufanya jumla kuwa Sh9.9 bilioni.