18 wapenya usaili RT,  Ikangaa, Isangi wajiondoa

Kuelekea uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), unaotarajiwa kufanyika Agosti 16 mwaka huu jijini Mwanza, wagombea 18 wamefaulu katika mchujo wa awali.

Mchakato huo umetawaliwa na matukio ya kushtua ikiwemo kujiondoa kwa nyota wa zamani wa riadha nchini, Juma Ikangaa  pamoja na rais aliyemaliza muda wake, Silas Isangi ambao walitangaza uamuzi huo wakiwa wmetiania kugombea urais.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa RT, Leonard Thadeo, kati ya wagombea 20 waliofika kwenye usahii, 18 wamepenya kuendelea na mchakato, huku wawili wakiwasilisha barua za kujiondoa.

“Wagombea Juma Ikangaa na Silas Isangi walifika mbele ya kamati na kutoa taarifa kwa maandishi kuwa wamejitoa kugombea nafasi ya rais,” amesema Thadeo.

Waliokidhi vigezo vya kuendelea ni pamoja na Angelus Likwembe, Rogath John Stephen, William Kallaghe na Nsolo Mlozi wote wakiwania urais, huku Baraka Sulus na Jackson Ndaweka wakiwania umakamu wa rais.

Wengine ni Noela Mafuru, Lwiza Msyani (Mwakilishi Wanawake), Christina Paga, Slyvia Rushokana, Shenya Imori, Alfredo Shahanga, Tullo Chambo, Michael Washa, Ibrahim Adam, Andrew Rhobi, Tabu Mwandu na Joshua Kayombo wanaowania nafasi nne za ujumbe wa kamati ya utendaji.

Akizungumza na Mwanaspoti, rais wa RT ambaye amemaliza muda wake Silas Isangi amesema ameamua kujiondoa ili kutoa nafasi kwa watu wengine wenye maono makubwa na mchezo wa riadha kuweza kuongoza.

“Nimeona tu kwamba sasa nipumzike, waje wengine pia, nikweli wengi wameshtuka kwamba nilikuwepo kwenye usahili, lakini hawakujua kwa sababu niliwaambia nitatumia dakika 15 tu,” amesema Isangi na kuongeza:

“Tusamehane, wacha waingie na wengine wafanye kazi pia, tuone riadha yetu inafika wapi nitatumikia hata TOC.”