Dah! Kwa Mkapa bado | Mwanaspoti

Muonekano wa mashabiki katika Uwanja wa Benjamin Mkapa siyo kama vile ambavyo ulitarajiwa kutokana na nyomi ya ilivyokuwa nje ya uwanja mapema leo kabla ya kuruhusiwa kuanza kuingia.

Kabla ya mageti kufunguliwa watu walijaa nje ya uwanja wakisubiri kuingia ili kushuhudia mechi kati ya Taifa Stars dhidi ya Burkina Faso inayotarajiwa kuchezwa saa 2:00 usiku, lakini baada ya kuruhusiwa hali siyo nzuri  kutokana na majukwaa mengi kuwa wazi.

Hadi kufikia saa 18:25 jioni upande wa Kaskazini ambako wanakaa mashabiki wa Simba kuna eneo kubwa ambalo viti havina watu kama ilivyo upande ule wa Kusini ambapo wanakaa mashabiki wa Yanga.

Mbali ya burudani mbalimbali ambazo zinaendelea katika uwanja huu zikipigwa nyimbo mbalimbali za wasanii wa muziki wa bongo fleva kumekuwa na muitikio mkubwa wa mashabiki wakifurahia burudani hiyo.

Mashabiki wanaendelea kuingia mdogomdogo kuongeza mwitikio wa Watanzania waliojitoa kuja kutoa sapoti kwa wachezaji wa Taifa Stars wanaocheza ligi ya ndani.