Azam FC, Yanga zaingia vitani

INAELEZWA kwamba uongozi wa Azam na Yanga umeingia katika vita nzito baada tu ya usajili wa beki ambaye pia ana uwezo wa kucheza kiungo mkabaji, Abubakar Nizar Othman ‘Ninju’, aliyesajiliwa na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025 akitokea JKU SC ya Zanzibar.

Ninju ametangazwa rasmi kujiunga na Yanga ambapo usajili wake umeibua sintofamu kubwa kwa sasa, baada ya mabosi wa Azam kudai nyota huyo ni mali yao halali, kwani kucheza kwake JKU msimu uliopita alikuwa kwa mkopo na bado ana mkataba nao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’, alisema nyota huyo ni mali yao na bado ana mkataba hadi mwaka 2027, hivyo kucheza JKU ilikuwa ni kwa mkopo kwa lengo la kumpa nafasi ya kulinda kipaji chake.

Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua uongozi wa Azam umefungua rasmi malalamiko yake katika Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kwa kile wanachodai Yanga imeenda kinyume kwa kumtambulisha mchezaji mwenye mkataba na timu nyingine.

“Wamefungua malalamiko yao kwa TFF ili kuishtaki Yanga kumsajili mchezaji ambaye bado ana mkataba na Azam. Suala hilo ni mwendelezo wa mikasa ya klabu kwa klabu kama ambavyo tumezoea kuona kila pale usajili unapofika,” kilisema chanzo hicho.

Kwa sasa Yanga inaendelea na maboresho ya kikosi chake kuelekea msimu ujao ambapo imeshasajili na kuwatambulisha wachezaji wapya saba ambao ni Balla Moussa Conte (CS Sfaxien), Offen Chikola (Tabora United), Abdulnassir Mohamed Abdullah ‘Casemiro’ (Mlandege FC), Lassine Kouma (Stade Malien), Andy Bobwa Boyeli (Sekhukhune United FC), Celestin Ecua (Zoman FC) na Abubakar Nizar Othman ‘Ninju’ (JKU).