TAKUKURU TEMEKE YAIBUA TUHUMA ZA RUSHWA KWA WATIA NIA UBUNGE CCM

Na Mwandishi Wetu | Nipashe | Agosti 2, 2025

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke inawachunguza watia nia wawili wa nafasi ya ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa tuhuma za kushawishi kutoa rushwa kwa wajumbe wa kura za maoni.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkuu wa TAKUKURU mkoani humo, Bw. Holle Makungu, alisema uchunguzi wa awali unaendelea dhidi ya watuhumiwa hao ambao majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi, huku wakiripotiwa kuwa wapo nje kwa dhamana.

“Taarifa hizi tayari zimewasilishwa kwa chama husika, na hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kutoyarejesha majina yao katika mchakato wa kura za maoni,” alisema Bw. Makungu.

Aliwataka wagombea na wapiga kura kufuata sheria za uchaguzi na kuepuka kushiriki katika vitendo vyovyote vya rushwa, akifafanua kuwa makosa ya uchaguzi yanayohusiana na rushwa ni pamoja na kutoa au kupokea fedha ili mtu ateuliwe, ajitoe au amuunge mkono mgombea mwingine, au kununua/kumuuzia mtu kadi ya mpiga kura.

Katika hatua nyingine, TAKUKURU Temeke imefanya ufuatiliaji wa miradi tisa ya maendeleo yenye thamani ya Sh. bilioni 7.42 inayotekelezwa katika sekta za elimu, afya, ujenzi na biashara.

Bw. Makungu alisema kuwa miradi mitatu kati ya hiyo ilibainika kuwa na dosari mbalimbali, ambapo ushauri wa kitaalamu ulitolewa na kutekelezwa na wakurugenzi wa Manispaa za Temeke na Kigamboni waliokuwa wasimamizi wa miradi hiyo.

Akielezea utekelezaji wa programu ya TAKUKURU Rafiki, alisema taasisi hiyo imetoa elimu kwa wananchi katika kata nane na kufanikisha utatuzi wa kero 65 kati ya 70 zilizowasilishwa, huku tano zikiendelea kushughulikiwa.

Alitaja baadhi ya changamoto kuwa ni ubovu wa miundombinu katika Soko la Mbagala Kizuiani, ambapo maboresho yanaendelea, hasa kwenye eneo la wauza samaki. Aidha, wafanyabiashara wa Soko la TAZARA waliomba kukamilishwa kwa ujenzi wa vyoo vipya, kazi ambayo inadaiwa kuwa inaendelea.

Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, TAKUKURU Temeke imepokea malalamiko 58, ambapo 40 yalihusu rushwa na 18 yalihusu masuala mengine. Kesi mbili zimefikishwa mahakamani, na jumla ya kesi 13 zinashughulikiwa na vyombo vya sheria kwa sasa.

Bw. Makungu alisema kuwa kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2025, taasisi hiyo imepanga kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya rushwa, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.

“Natoa wito kwa wananchi wote kuepuka kushiriki katika vitendo vya rushwa, na kutoa taarifa wanapobaini viashiria vyake kupitia ofisi zetu au kupiga simu bure namba 113,” alihitimisha.