Kocha mpya Yanga ashuhudia mavitu ya Mzize Stars

KOCHA mpya wa Yanga, Romain Folz ni miongoni mwa watu waliofika katika Uwanja wa Mkapa kushuhudia mchezo wa ufunguzi kati ya Tanzania na Burkina Faso katika ufunguzi wa mashindano ya CHAN.

Kocha huyo ameambatana na benchi lote la wasaidizi wake ambao ni kocha wa makipa, mkurugenzi wa benchi la ufundi na kocha wa viungo wote wakiwa wapya ndani ya kikosi cha Yanga.

Katika mchezo huo, straika wa Yanga, Clement Mzize alionekana kuwatesa mabeki wa Burkina Faso akiwachachafya atakavyo.

Folz ambaye atakuwa na kibarua cha kuhakikisha Yanga inatetea taji la Ligi Kuu Bara alifika uwanjani akiwa sambamba na Meneja wa Yanga, Walter Harson.

Mara baada ya kutazama mpira kwa muda akiwa jukwaa  la VIP, Folz aliondoka uwanjani dakika ya 78 akiacha mchezo bado unaendelea.

Mchezo huo wa wa kwanza kwa michuano ya CHAN 2024 umemalizika kwa Tanzania kushinda mabao 2-0 yaliyofungwa na Abdul Suleiman Sopu kwa njia ya mkwaju wa penalti pamoja na Mohamed Hussein kwa kichwa.