Riadha Dar kuanza na ofisi

SIKU chache baada ya kuingia madarakani, Mwenyekiti wa Chama cha Riadha Dar Es Salaam (DAA), Amani Ngoka amefunguka moja ya mikakati waliyonayo ni kuhakikisha wanapata ofisi rasmi ya chama hicho.

Alisema DAA imekosa ofisi kwa muda sasa, hivyo kusababisha kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi na kama watapata itasaidia katika kuratibu shughuli zote zinazohusu maendeleo ya mchezo huo wa riadha kwa urahisi.

Ngoka aliongeza pia wamepanga kushirikiana na shule mbalimbali za Mkoa wa Dar es Salaam ili kutafuta vipaji vya vijana ambao watakuja kuleta ushindani kwa mikoa kama Arusha, Manyara na Singida ambazo ndizo zinaonekana kufanya vizuri katika mchezo huo.

“Kwa sasa nguvu zote tunaelekeza katika kutafuta ofisi, tukishapata sasa tunaingia shuleni kwani uko kuna watoto wengi wenye vipaji ambao wanaweza kuja kuwa kina Simbu, Sakilu wa baadae,” alisema Ngoka.

Aliweka wazi watakuwa na jukumu la kuanzisha programu za riadha shuleni ambazo zitawezesha wanafunzi kushiriki katika mashindano mbalimbali.

Kocha huyo wa riadha wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) alisema pia wanajipanga kuandaa mafunzo maalum kwa makocha, akiamini yatasaidia kuzalisha walimu wengi ambao watazalisha wanariadha wa baadae.

Uchaguzi wa DAA ulifanyika Julai 31 mwaka huu ambapo Amani Ngoka alichaguliwa katika nafasi ya Mwenyekiti, huku Elizabeth Tungaraza (makamu mwenyekiti), Felix Chunga (katibu), Mwalimu Juma Ally (katibu msaidizi), Monica Luswaga, Habib Shamte, Difna Chailla, Tausi Irunde, na Christian Yahhi, walichaguliwa nafasi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji.