RAIS wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Silas Isangi ameweka wazi sababu za kujiondoa katika kinyanganyiro cha kutetea kiti chake.
Isangi ni miongoni mwa wagombea 20 waliokuwa katika mchakato wa usaili wa Kamati ya Uchaguzi wa RT baada ya kurejesha fomu za kugombea katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Agosti 16 mwaka huu, jijini Mwanza.
Ingawa alifika katika mchujo huo, Isangi alifanya maamuzi ya ghalfa kwa kuandika barua ya kujiondoa, nyota wa zamani wa riadha Tanzania, Juma Ikangaa aliyeonyesha nia ya kutaka kugombea Urais, pia alijiondoa katika mchakato huo.
Akizungumza na Mwanaspoti, kiongozi huyo alisema ameamua kuachia nafasi ili kuwapa fursa wengine wenye mawazo mapya katika riadha.
“Nimeona nipumzike, waje wengine pia, ni kweli wengi wameshtuka nilikuwepo kwenye usaili, lakini hawakujua kwa sababu niliwaambia nitatumia dakika 15 tu,” alisem Isangi na kuongeza;
“Tusamehane, wacha waingie na wengine wafanye kazi, tuone riadha yetu inafika wapi nitatumikia hata TOC.”
Aliongeza japo wengi walitamani aendelee kuongoza, lakini kwa maendeleo ya mchezo wa riadha amejiweka pembeni, huku akiamini rais atakayechaguliwa Agosti 16 atakuwa mtu sahihi.
Majina 18 yaliyopita katika usaili na sasa wanakwenda kugombea nafasi mbalimbali za uongozi wa RT, ni Angelus Likwembe, Rogath John Stephen, William Kallaghe na Nsolo Mlozi, wote wakiwania Urais, huku Baraka Sulus na Jackson Ndaweka upande wa Makamu wa Rais.
Wengine ni Noela Mafuru, Lwiza Msyani (Mwakilishi Wanawake), Christina Paga, Slyvia Rushokana, Shenya Imori, Alfredo Shahanga, Tullo Chambo, Michael Washa, Ibrahim Adam, Andrew Rhobi, Tabu Mwandu na Joshua Kayombo wanaowania nafasi nne za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.