Mido Mkenya, Sowah wainogesha kambi

KIKOSI cha Simba leo Jumatatu kinaingia siku ya tano kikiwa kambini katika jiji la Ismailia, Misri kujiandaa na msimu mpya na kikosi hicho kimepokea kundi lingine la wageni na wenyeji wakiwa huko na kuna mashine mbili mpya zilizoongeza mzuka.

Msafara wa kwanza wa Simba uliondoka nchini Jumatano ukiwa na mastaa wapya na wa zamani sambamba na benchi la ufundi chini ya kocha Fadlu Davids.

Kundi la pili la msafara wa kikosi hicho kiliondoka jana Jumapili alfajiri likiwa na wachezaji na baadhi ya maafisa wa timu hiyo tayari kwa kuungana na kundi la kwanza lililotangulia siku tano zilizopita.

Wachezaji ambao wameondoka jana ni pamoja na washambuliaji Jonathan Sowah, Kibu Denis na viungo Mohammed Bajaber, Mzamiru Yassin, Semfuko Charles, Saleh Karabaka, Morice Abraham na Alassane Kante.

Sowah, Bajaber kiungo fundi kutoka Kenya, Kante, Morice na Semfuko hizo ni mashine mpya ambazo zinakwenda kukutana kwa mara ya kwanza na timu hiyo kuanza mapya ndani ya kikosi.

Wachezaji hao walichelewa kufuatia kusubiri hati ya kuingia nchini Misri ambazo zilikamilika Ijumaa wiki iliyopita.

Kuongezeka kwa wachezaji hao kutaongeza mzuka katika kambi hiyo, kutokana na wachezaji watazidi kuongeza idadi kufuatia awali kuwa na wachezaji wachache.

Taarifa kutoka ndani ya kambi hiyo, zinasema kocha Fadlu hakuwa anataka timu hiyo iungane kwa makundi ambapo itachelewesha kukamilika kwa maandalizi yao, hivyo kuungana pamoja kumpa kazi rahisi ya kusuka mbinu na mipango yake kwa msimu mpya wa mashindano.

Simba itakuwa kambini kwa wiki mbili hadi nne kujiandaa kwa msimu mpya, ambapo inarudi Ismailia kwa mara ya pili kama ambavyo ilifanya msimu uliopita.

Wachezaji wengine ambao hawajajiunga na kambi hiyo ni pamoja na wale wanaoshiriki Fainali za Mataifa Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN walioko kikosi cha Taifa Stars.