Huko Yanga bado mmoja tu!

YANGA imeshaanza maandalizi ya msimu mpya wa mashindano kwa mwaka 2025-26 na jana Jumapili mazoezi ya timu hiyo yalisitishwa kidogo kisha kufanyika kikao kizito kati ya mabosi wa klabu hiyo na mastaa wa timu hiyo huku mashine moja tu ikikosekana ukiacha wale walioko timu ya Taifa.

Kikao hicho kiliitishwa na Rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said akiwa na wasaidizi wake na kubwa ni kuwapa msimamo na malengo wachezaji wapya na wale waliosalia katika timu hiyo ambao msimu uliopita waliiwezesha timu hiyo kukomba mataji matano kwa mpigo ikiwamo kutetea Ligi Kuu na FA.

Mbali na wachezaji wa timu hiyo pia benchi zima la ufundi chini ya kocha Romain Folz nalo limehusika katika kikao hicho.

Mkutano huo wa pamoja ulifanyika asubuhi ya jana katika hoteli moja kubwa pale katikati ya Jiji la Dar es Salaam ambapo Hersi aliwakaribisha wachezaji wapya wa timu hiyo pamoja na makocha wao kisha kuwapa msimamo juu ya malengo ya timu yao kwa msimu ujao.

“Tumeambiwa namna msimu unavyoweza kuwa mgumu lakini kikubwa tutakaokwenda kuufanya kuwa rahisi ni sisi wachezaji,” alisema mmoja wa mastaa wa timu hiyo ambaye amesalia kikosini na kuongeza;

“Bosi (Hersi) ametuambia kabisa kwa timu iliyotengenezwa msimu huu hakuna kitu wanataka kusikia zaidi ya kuendeleza mafanikio haya. Mashabiki wanataka makombe na wao watalisimamia hilo na sisi ndio tutakaotakiwa kufanikisha, Yanga haina shida ya fedha tutalipwa kwa wakati bonasi, mishahara na malipo mengine kama ilivyokuwa nyuma.”

Katika mkutano huo mastaa hao wakiwamo wapya waliosajiliwa na kutambulishwa walihudhuria, lakini mchezaji ambaye hayupo kwenye kikosi cha Taifa Stars ambaye hajaripoti ni mmoja pekee Pacome Zouzoua.

Pacome anatarajiwa kuingia nchini ndani ya siku mbili zijazo baada ya kuomba ruhusa ya kuchelewa kidogo akiwa kwao Ivory Coast.

Yanga imewaongeza wapya saba wakiwamo wageni watano ambao wameshatambulishwa Celestin Ecua, Lassine Kouma, Andy Boyeli, Moussa Bala Conte, wazawa wakiwa Offen Chikola, Abubakar Othman, Abdulnasir Mohammed.

Pia wamo Mohamed Doumbia, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambao nao tayari wameshasainishwa wakisalia kutambishwa tu kwa sasa, huku ikielezwa dirisha la usajili litafungwa na beki wa kati anayefuatiliwa kupitia fainali za CHAN 2024 inayoendelea katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.