BAADA ya Simba kumpa mkono wa kwaheri wiki chache zilizopita mshambuliaji raia wa Kenya, Jentrix Shikangwa inadaiwa yupo njiani kurejeshwa kikosini kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) na michuano mingine ya ndani ya soka la wanawake.
Julai 15 mwaka huu, Simba ilitangaza kuachana na mshambuliaji huyo wa zamani wa Vihiga Queens na timu ya taifa ya Kenya, Harambee Starlets, akiwa miongoni na nyota 13 walioitumikia msimu uliopita.
Shikangwa ndani ya misimu mitatu aliyocheza Simba, msimu wa kwanza tu aliipa timu hiyo ubingwa na akaibuka mfungaji bora akiweka kambani mabao 17, uliofuata akamaliza na mabao manane akicheza mechi nane na huu kamaliza na mabao 24.
Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa Simba Queens, aliliambia Mwanaspoti wameamua kumrejesha kikosini kutokana na uhitaji wake na kile alichokifanya ndani ya misimu mitatu.
“Kulikuwa na changamoto kidogo ya uamuzi na ni kama tulikurupuka, lakini maoni ya mashabiki mitandaoni yametuamsha kwa sababu wao pia wanahusika na hii timu,” alisema kiongozi huyo na kuongeza:
“Viongozi wakubwa waliuliza shida nini, tukasema mchezaji alitaka kiasi kikubwa cha pesa, wakasema mpatieni hiyo fedha kwa sababu ni mchezaji muhimu kwetu na amefanya makubwa.”
Msimu uliopita Simba ilitemeshwa taji ililokuwa ikilitetea na maafande wa JKT Queens na kufanya sasa timu hizo kulingana kwa kutwaa mara nne kila moja tangu Ligi hiyo ilipoasisiwa mwaka 2016.