KLABU ya Mtibwa Sugar inakaribia kuipata saini ya kiungo wa maafande wa Tanzania Prisons, Ezekia Mwashilindi, baada ya nyota huyo kufanya mazungumzo na timu hiyo, ambayo hadi sasa yanaendelea vizuri ili kukitumikia kikosi hicho msimu ujao.
Nyota huyo wa zamani wa Singida BS, kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Prisons, ambapo kikosi hicho cha maafande kinafanya mazungumzo ya kumuongezea, japo mwenyewe anatafuta changamoto sehemu nyingine mpya.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru, alisema licha ya kimya kingi kwa kikosi hicho, ila mashabiki watarajie mambo makubwa, kwa sababu wanataka kufanya mambo yao kwa weledi na kwa kuzingatia mahitaji pia.
“Sisi hatushindani na wengine ili kujionyesha tunasajili sana, tunafanya mambo yetu kimyakimya lakini tukizingatia yale yote mahitaji yetu muhimu, kikubwa niwasihi mashabiki zetu wawe na subra na watajionea mambo mazuri,” alisema Thobias.
Hata hivyo, licha ya kauli ya Kifaru, ila Mwanaspoti linatambua Mwashilindi amefikia makubaliano ya kusaini mkataba wa mwaka mmoja wenye kipengele cha kuongeza mwingine, japo kilichobaki ni kuingiziwa fedha ili asaini kuichezea msimu ujao.
Mbali na Mwashilindi kukaribia kujiunga na timu hiyo huku Prisons ikimshawishi kuongeza mkataba mpya, aliyekuwa beki wa kushoto wa Namungo na Azam, Edward Charles Manyama anakaribia pia kujiunga nao baada ya kuondoka Singida Black Stars.
Timu hiyo iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, imerejea tena Ligi Kuu ikiwa ndio mabingwa wa Ligi ya Championship baada ya kumaliza vinara kwa kuwa na pointi 71, ikiungana na Mbeya City iliyorejea pia kufuatia kushuka daraja msimu wa 2022-2023.