Pamba Jiji yamkomalia Kelvin Nashon

UONGOZI wa Pamba Jiji uko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa kiungo wa Singida Black Stars, Kelvin Nashon, baada ya kikosi hicho kushindwa kufikia makubaliano ya kuipata saini ya nyota huyo katika dirisha dogo la Januari 2025.

Nyota huyo alishindwa kufikia makubaliano binafsi na kikosi hicho katika dirisha dogo, ingawa kwa sasa mazungumzo yanaendelea vizuri, huku Mwanaspoti likitambua wazi mchezaji huyo ameruhusiwa kutafuta timu nyingine atakayoichezea kwa msimu ujao.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza Pamba haikuwa na mpango tena na nyota huyo ingawa baada ya ujio wa kocha Francis Baraza amependekeza kusajiliwa, jambo ambalo kwa sasa kilichobakia ni makubaliano ya maslahi binafsi baina yao.

“Makubaliano yaliyopo ni ya kumpata kwa mkopo na sio moja kwa moja kwa sababu hatuwezi kulipa gharama za kuvunja mkataba wake na Singida uliobakia, mazungumzo bado yanaendelea vizuri na tutakamilisha dili hilo mapema,” kilisema chanzo hicho.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Pamba, Ezekiel Ntibikeha alisema kinachoendelea kwa sasa ni tetesi tu na sio uhalisia, ingawa baada ya kukamilisha taratibu zote wataanza kutangaza usajili wa mastaa wapya watakaokuwa nao.

Pamba ina uhusiano mzuri pia wa kupata wachezaji kutoka Singida, kwa sababu katika dirisha dogo la Januari 2025, ilinasa saini za kipa, Mohamed Kamara na washambuliaji watatu wakiwamo, Habib Kyombo, Hamad Majimengi na Abdoulaye Yonta Camara.

Kikosi hicho kimenasa saini ya mastaa mbalimbali, wakiwemo Abdallah Iddi ‘Pina’ aliyekuwa mfungaji bora wa Mlandege FC ya Zanzibar msimu uliopita, John Mbise (Geita Gold), Amos Kadikilo (Fountain Gate) na Najim Mussa kutokea Tabora United.