KADRI mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani yakianza leo, majina ya mastaa kadhaa yamekuwa yakikumbukwa lakini kubwa zaidi ni la mwamba wa Morocco Ayoub El Kaabi aliyetumia michuano hii kama njia ya kutua Ulaya na sasa imebaki historia.
El Kaabi, mshambuliaji wa Morocco, alivuma kupitia CHAN 2018, na mafanikio hayo yakamfungulia njia ya kuwa staa mkubwa wa kimataifa kwa sasa.
Msimu huo alitwaa Kiatu cha Dhahabu na Mchezaji Bora wa CHAN 2018, lakini sasa amekuwa akitajwa kama mmoja kati ya wachezaji wakubwa zaidi duniani akiwa ameshakuwa mfumgaji bora wa Ligi Kuu ya Ugiriki na Mchezaji Bora wa Fainali ya UEFA Europa Conference League.
Safari ya staa huyu ni mfano kwa vijana wengi, haswa ambao watakuwa kwenye Uwanja wa Mkapa leo kushiriki kwenye mchezo mkali wa ufunguzi wa michuano hiyo, kila atakayeweka juhudi mbele, itakuwa ni nafasi nzuri kwake kufanikiwa kutoka barani Afrika na kwenda Ulaya, Asia au Amerika kuionyesha dunia kuwa soka linalipa.

Katika mashindano ya CHAN 2018 yaliyofanyika Morocco, El Kaabi alivunja rekodi kwa kufunga mabao tisa katika mechi sita pekee, akitwaa tuzo ya Mfungaji Bora na Mchezaji Bora wa mashindano. Morocco ilitwaa ubingwa kwa kuichapa Nigeria 4-0 katika fainali, huku El Kaabi akifunga bao la tatu dakika ya 73.
“Nilikuwa na hisia nyingi, nilipoona jitihada zangu hatimaye zimezaa matunda,” alisema El Kaabi akitafakari mafanikio yake. Mabao yake tisa bado yanashikilia rekodi ya mabao mengi zaidi katika michuano hii ya CHAN.
Staa huyo alizaliwa Casablanca mwaka 1993, lakini alishindwa kuendelea na shule akiwa na miaka 15 pekee na kuamua kuingia kwenye kazi ya useremala na kucheza soka ya mtaani ni dhihirisho la mwanzo mgumu wa maisha yake.
Akiwa mtaani kwao alijiunga na timu ya Racing Casablanca alipofunga mabao 25 katika mechi 33, ndipo akaanza kuvutia macho ya wakubwa, na hatimaye kusajiliwa na RS Berkane ya nchini kwao na kwa sasa ndiyo mabingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Akiwa na Berkane, mshambuliaji huyo aliitwa kwenye kikosi cha CHAN 2018 cha nchini kwao. Mabao yake dhidi ya Guinea (hat-trick), na Nigeria katika fainali, yalimweka kwenye ramani ya mwanasoka bora zaidi ya mashindano hayo ambayo yalijaza makocha, maskuti na watu wengine mashuhuri kutoka kwenye mataifa mbalimbali na baadhi walianza kumfuatilia kwa karibuni.
Klabu kadhaa za China, wakati huo zilianzia kuchipua kwa kasi kubwa kwenye uwekezaji wa soka duniani na zikamwona kama lulu. Hakuchelewa akajiunga na Hebei China Fortune kwa mkataba mnono wa fedha ndefu, japo kimaendeleo haukuwa wa mafanikio makubwa kutokana na asili ya soka la nchi hiyo.
Alikaa muda mchache na kurejea Morocco na alijiunga na Wydad Casablanca mwaka 2019 na kuwa mfungaji bora wa ligi ya Morocco msimu wa 2020–21.
Baada ya hapo, aliondoka na kwenda Uturuki akajiunga na Hatayspor, ambako alifunga mabao 26 katika mechi 53 na kuanza kuishangaza dunia kama kweli ni mchezaji yule ambaye aliwika kwenye CHAN.

Mwaka 2023, El Kaabi aliondoka kwenye timu hiyo na kujiunga na miamba ya Ugiriki, Olympiacos, ambapo msimu mmoja tu, duniani ilimtambua msimu wa 2023–24, akiwa kwenye timu hiyo yenye mastaa wakubwa duniani alifunga mabao 11 katika mechi tisa za UEFA Europa Conference League, akifunga hat-trick dhidi ya Aston Villa katika nusu fainali, na bao la ushindi dhidi ya Fiorentina katika fainali, akiwapa Olympiacos taji lao la kwanza la Ulaya katika historia yao.
Kama alivyofanya kwenye CHAN 2008 ndivyo alivyofanya kwenye UEFA akiweka rekodi ya mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi katika hatua ya mtoano ya UEFA, akiwapiku wakali kama Karim Benzema, Cristiano Ronaldo na Radamel Falcao.
Mwisho aliibuka mchezaji bora na mfungaji bora wa mashindano, akiwa Mwafrika wa kwanza kufunga mabao zaidi ya 10 katika toleo moja la UEFA Conference League.
Kwa ujumla, alifunga mabao 14 katika mashindano ya UEFA msimu huo idadi kubwa zaidi kuwahi kufikiwa na mchezaji wa kutoka barani Afrika, katika msimu mmoja wa klabu za UEFA. Pia alikuwa mchezaji wa kwanza kufunga idadi ya mabao hayo tangu Lionel Messi alipofanya hivyo msimu wa 2011–12.

Mwanzoni mwa mwaka huu 2025, El Kaabi alikuwa ameweka historia nyingine kwa kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Olympiacos katika michuano ya UEFA akiwa na mabao 21 katika mechi 26. Aliongoza timu kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ugiriki, akifunga mabao mengi zaidi msimu huo na kuteuliwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi na Mchezaji Bora wa Kigeni nchini humo.
Kocha wake, Jose Luis Mendilibar, alisema: “Huyu ni mchezaji wa kipekee. Njaa yake ya mafanikio na umakini wake, ndio chanzo cha mafanikio yetu.”

Leo hii, akiwa na umri wa miaka 32, El Kaabi ni miongoni mwa mastraika wa kutegemewa barani Ulaya. Safari yake ni kielelezo halisi cha jinsi CHAN inavyoweza kumbadilishia maisha mchezaji wa ndani.
Mashindano haya, yaliyoundwa kwa ajili ya wachezaji wa ligi za ndani, yamethibitisha kuwa ni jukwaa la ndoto kuwa halisi. leo ikiwa CHAN inaanza kwa nchi za Afrika Mashariki, wachezaji wengi watakuwa wakitamani kufuata nyayo za El Kaabi kuanzia mechi za ndani hadi kwenye majukwaa ya kimataifa.
Tayari ni mchezaji mwenye heshima kubwa Morocco ambapo ameshafunga mabao 16 kwenye timu hiyo katika michezo 42 aliyoitumikia. Kila mmoja apambane kwa wakati wake.