Sare yambeba kipa Madagascar | Mwanaspoti

KIPA wa Madagascar, Michel Ramandimbozwa aliibuka shujaa baada ya kuiongoza timu yake kulazimisha suluhu dhidi ya Mauritania, licha ya kucheza wakiwa pungufu kutokana na kuonyeshwa kwa kadi nyekundu ya kwanza katika mashindano hayo.

Ramandimbozwa, ambaye aliibuka kuwa Mchezaji Bora wa mechi, aliwavutia wengi kwa ubora wake langoni na alifanya kazi ya ziada kuokoa mashambulizi ya Mauritania.

Licha ya presha kubwa ya Mauritania hasa kipindi cha pili, Ramandimbozwa alionyesha utulivu mkubwa na kufanya maamuzi sahihi kwenye nyakati muhimu, ikiwa ni pamoja na kuokoa hatari ya wazi kutoka kwa Moulay Ahmed Khalil.

Kadi nyekundu ya nahodha Dax kabla ya mapumziko ilitibua mipango ya Madagascar ambao wapo kundi moja na Taifa Stars, lakini badala ya kuporomoka, walijipanga upya na kupigania pointi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Akizungumza baada ya mechi, Ramandimbozwa alisema: “Namshukuru Mungu kwa matokeo haya. Tuliteseka kwa kuwa pungufu lakini tuliendelea kupigana. Umoja wetu ndiyo uliotusaidia kuhimili presha.”

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 alikiri matokeo hayo si tu yamewapa alama, bali pia yamewaweka katika hali nzuri kisaikolojia kwa mechi zijazo, hasa ukizingatia kuwa hiyo ilikuwa mechi yao ya kwanza.

Ramandimbozwa aliongeza anatambua matarajio ya Wamalagasi kwa timu yao, na kuahidi kuendelea kujitoa kwa ajili ya taifa lao: “Nina furaha kwa kile tulichokifanya, lakini hii ni hatua ya kwanza. Tunalenga kuendelea kuonyesha kiwango bora zaidi.”

Matokeo hayo yameifanya Stars kuendeleza kuongoza msimamo wa Kundi B ikiwa na pointi tatu na mabao mawili huku wakifuata Madagascar na Mauritania wenye pointi moja kila mmoja, Afrika ya Kati ambayo bado haijacheza ipo nafasi ya nne kisha Burkina Faso.