Morocco ubabe unaendelea CHAN | Mwanaspoti

Timu ya taifa la Morocco, Atlas Lions, imeanza kampeni yake ya kutafuta taji la tatu la mashindano ya CHAN 2024 kwa kishindo baada ya kuibuka na ushindi jana, Jumapili wa mabao 2-0 dhidi ya Angola kwenye Uwanja wa Nyayo, Nairobi.

Bao la kwanza la Morocco lilifungwa na Imad Riahi katika dakika ya 29 kabla ya Kinito wa Angola kujifunga katika dakika ya 81 na kuipa Morocco ushindi.

Morocco, ambayo imeshawahi kutwaa taji hili mara mbili (2018 na 2020), iliingia kwenye mechi hii ikiwa na rekodi ya kutopoteza mechi 13 mfululizo kwenye CHAN, na haikusita kuonyesha kiwango chake tangu dakika za awali kwa kumiliki mpira na kutengeneza nafasi nyingi.

Kocha mkuu Tarik Sektioui aliongoza kikosi chake kilichokuwa na mabadiliko mengi kwa kuonyesha nidhamu ya kiufundi, huku nyota kama Mohamed Hrimat, Riahi, Anas Bach na Marouane Louadni wakiliweka lango la Angola kwenye wakati mgumu kabla ya mapumziko.

Angola kwa upande wao walijitahidi kuonyesha dalili za kurudi mchezoni kupitia mashambulizi ya hapa na pale yakiongozwa na Jo Paciencia na Aguinaldo Matias, lakini kipa wa Morocco El Mehdi Al Harrar alikuwa kikwazo kwao.

Kipindi cha pili kilishuhudiw3a Morocco ikiendelea kutawala, huku Angola wakifanya mabadiliko kadhaa kujaribu kubadili mchezo. 

Hata hivyo, ilikuwa ni Morocco waliopata bao la pili katika dakika ya 81 baada ya Youness El Kaabi kuingia uwanjani na kuchangia kwa kiasi kikubwa bao la kujifunga kwa Kinito, aliyekuwa akijaribu kuokoa. 

Hii ilikuwa ni mara ya tano kwa Angola kushiriki CHAN lakini hawajawahi kushinda mchezo wa ufunguzi katika historia yake kwenye michuano hiyo, na sasa ina kazi kubwa ya kuibuka kutoka kundi hilo gumu linalowajumuisha pia wenyeji Kenya na Zambia.

Kwa Morocco, ushindi huu unaimarisha nafasi yao na kuendeleza rekodi yao ya kutopoteza mechi za makundi tangu CHAN ilipoanzishwa. Mechi yao inayofuata itakuwa dhidi ya Kenya, wakati Angola wakikabiliana na Zambia katika harakati za kujiokoa.