KWA mujibu wa tetesi za usajili nchini Ufaransa, inaelezwa mshambuliaji wa Kitanzania, Mbwana Samatta yuko kwenye hatua za mwisho kujiunga na Le Havre ya Ligi Kuu Ufaransa.
Samatta ameachana na PAOK ya Ugiriki miezi michache iliyopita baada ya kuhudumu kikosini hapo kwa takribani misimu miwili akifunga mabao sita kwenye mechi 41.
Mbali na Le Havre nyota huyo ana ofa mbili timu kutoka Ligi Kuu Saudia na Southampton inayoshiriki Ligi ya Championship England.
Gazeti la Paris Normandie limeandika kuwa nyota huyo wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ amewasili Ufaransa jana Jumatatu kukamilisha taratibu za kumalizana na timu hiyo inayoshiriki Ligue 1, ambako klabu ya PSG yenye mastaa kama Ousmane Dembele na Achraf Hakimi, ndio mabingwa watetezi.
Liliongeza kuwa usajili huo ni chaguo la kocha wa timu hiyo, Didier Digard, aliyetaka kuongezewa mshambuliaji mwenye uzoefu aina ya Samatta.
“Kocha anatarajiwa kufurahia ujio wa Samatta kutokana na mahitaji ya timu na ameomba kuongezewa nguvu kwenye eneo la ushambuliaji na amempendekeza nyota huyo,” ilisema taarifa hiyo.
Inaelezwa Samatta anakwenda kuchukua nafasi ya Andre ‘Dede’ Ayew na Ahmed Hassan, washambuliaji walioondoka kikosini hapo msimu uliopita.
Kama dili hilo litakamilika, Samatta ataandika historia nyingine ya kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu Ufaransa.
Kabla ya hapo, nyota huyo aliichezea Genk na Royal Antwerp ya Ubelgiji. Mwaka 2016, ndani ya misimu minne akiwa Genk, alifunga mabao 76 na kutoa pasi 20 za mabao katika mechi 191.
Aling’ara zaidi msimu wa 2018-2019 ambapo aliiwezesha Genk kutwaa ubingwa wa Ligi ya Ubelgiji na akaibuka mfungaji wa pili bora kwa mabao 23.
Mwaka 2020, alisajiliwa na Aston Villa na kuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu England, lakini hakufanikiwa kung’ara katika ligi hiyo, akifunga mabao mawili katika mechi 16, likiwamo moja la fainali ya Kombe la Ligi dhidi ya Manchester City 2-1.
Baadaye alitimkia Fenerbahçe ya Uturuki mwaka 2021, akacheza mechi 33 akifunga mabao sita, kisha akatolewa kwa mkopo kwenda Royal Antwerp na baadaye Racing Genk. Mwaka 2023 alijiunga na PAOK.