BAADA ya sintofahamu kama aliyekuwa beki wa Namungo, Antony Mligo anaweza kujiunga na Simba dirisha hili kutokana na kuwa na mkataba na waajiri wake sasa ni rasmi amethibitisha kuwa ni Mnyama baada ya kuaga.
Simba iliiomba Namungo kumtazama mchezaji huyo kabla ya kumsajili jambo ambalo lilifanyika na sasa ni rasmi nyota huyo ataitumikia Simba msimu ujao.
Kupitia mtandao wa kijamii wa beki huyo ameandika: “Kwanza kabisa natoa shukrani zangu za dhati kwa wachezaji wenzangu kwa ushirikiano mzuri ndani pamoja na nje ya uwanja. Tulikuwa pamoja na kupambana kwa hali na mali katika kila nyakati furaha na huzuni tulivuka pamoja tukiwa imara.
“Napenda kulishukuru benchi la ufundi, viongozi wa timu, mashabiki na wapenzi wa Namungo FC kwa kuwa pamoja ndani ya mwaka mmoja tukiipambania nembo ya timu pamoja na malengo ya timu iliyojiwekea katika msimu mzima.”
Mchezaji huyo amedai inamuwia ugumu kuiaga familia aliyoishi nayo vizuri kwa upendo na amani wakati wote, lakini hana jinsi kwenda kupata changamoto sehemu nyingine akiamini watakutana wakati mwingine na amewatakia kila la heri katika msimu ujao 2025-2026.
Mlingo kujiunga na Simba anaenda kuziba pengo la Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye amendoka klabuni hapo baada ya kuitumikia kwa miaka 12 na anatajwa kujiunga na Yanga.