HUKO miluzi ni mingi kuhusiana na nyota wa Simba, Elie Mpanzu, ambako mijadala mbalimbali inaendelea wakati huu ambao ishu za usajili katika timu mbalimbali zimetaladadi, ambapo mastaa kibao wanabadili timu huku wapya wakisajiliwa kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano ndani na nje ya nchi.
Na nyuma ya mijadala inayoendelea kuna winga ambaye pia ni kiungo mshambuliaji wa Simba, Mpanzu, akidaiwa kwamba hajatia timu iliko kambi ya Wekundu wa Msimbazi kule Ismailia nchini Misri, na kwamba hata simu yake inadaiwa haipatikani inapopigwa.
Lakini, licha ya kuwepo kwa tetesi mbalimbali za Mpanzu kutopatikana hewani na kushindwa kujiunga na wenzake kambini, taarifa ambazo Mwanaspoti imepenyezewa ni kwamba nyota huyo anatarajia kutua Ismailia ndani saa 24 zijazo.
Awali, Mpanzu ilielezwa angetua Ijumaa wiki iliyopita, lakini ikashindikana na kudaiwa aliomba udhuru akiwa kwao na angetua juzi Jumapili ili kuondoka na kundi la pili la wachezaji wakiwamo kina Jonathan Sowah na wenzake, lakini alikwama na kuzua sintofahamu hiyo.
Juzi na jana kumekuwa na tetesi mbalimbali katika mitandao ya kijamii ikionyesha kuwa kiungo huyo hapatikani na huenda akajiunga na wapinzani wa Simba wakati wowote kuanzia sasa, lakini kigogo mmoja wa klabu hiyo, alilithibitishia Mwanaspoti, ndani ya siku moja kiungo huyo atakuwa ameshatua kambini kujiunga na wenzake kwa maandalizi ya msimu mpya wa mashindano wa 2025-26.
Mpanzu alijiunga na Simba katika dirisha dogo la usajili la msimu uliopita na kuonyesha kiwango cha juu ambapo alifunga mabao manne na kutoa asisti sita kwenye Ligi Kuu na kung’ara pia katika mechi za kimataifa ambapo Simba ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kigogo mmoja aliyepo na Simba kambini huko Misri alilithibitishia Mwanaspoti kuwa Mpanzu ameshaanza safari na ndani ya saa 24 mashabiki watarajie kuona picha zake akiwa na kikosi hicho kilichomaliza katika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu msimu uliopita.
“Hata sisi tunafuatilia kila kitu, Mpanzu ana mkataba na Simba na aliomba ruhusa maalum, alipewa na anatakiwa ndani ya saa 24 kutoka leo (jana) awe ameshafika kambini, siyo ajabu hata leo akafika kwa kuwa ameshaanza safari ya kuja hapa Misri kuungana na wenzake,” amesema kigogo huyo aliyeomba kuhifadhiwa jina gazetini aliyeongeza:
“Tunafahamu kuna majaribio mengi yanafanyika, lakini ni suala ambalo haliwezekani kwa kuwa huyo ni mchezaji mkubwa anayejiheshimu na anajua umuhimu wa mkataba wake, shabiki wa Simba hatakiwi kuwa na presha anatakiwa kuamini kuwa huyu ni mchezaji halali wa Simba.”
Hata hivyo, kigogo huyo alisema bado timu hiyo haijamaliza usajili kwa kuwa kuna wachezaji wengine ambao Simba bado inawataka na bado haijamalizana nao, hivyo mashabiki waendelee kusubiri mambo makubwa yanakuja.
Chanzo hicho kilisema wachezaji wa Simba watakuwa wanafika kambini baada ya kukamilisha taratibu za viza, kulingana na nchi husika wanazotokea, hivyo wapo wengi ambao bado hawajafika kambini, ukiachana waliopo timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa ajili ya majukumu ya CHAN 2024.
“Kwanza Simba bado inaendelea kufanya usajili, anayekamilisha ishu ya viza moja kwa moja anatakiwa ajiunge na kambi ndiyo maana nasisitiza hatuwezi kujibu kila upepo na kuhusu simu kutopatikana, kama wenyewe hawampati sisi tunampata na ni mchezaji aliyepo katika mipango ya Simba, hivyo hauzwi wala haondoki.”
Hadi sasa Simba imeshawatambulisha wachezaji wapya watano akiwamo Mohamed Bajaber kutoka Kenya, Alassane Kante raia wa Senegal, Jonathan Sowah pamoja beki Msauzi, Rushine de Reuck, huku wazawa wakiwa ni wawili Morice Abraham, Charles Semfuko.