Mahakama ilivyobatilisha uamuzi kesi ya Sheria ya Mawakili

Dar es Salaam. Mahakama ya Rufaa imebatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu uliotolewa na jaji mmoja aliyesikiliza na kuamua pingamizi la awali katika kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na wakili Mpale Mpoki.

Uamuzi uliotolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa Julai 31, 2025 umesema jaji huyo wa Mahakama Kuu hakuwa na mamlaka ya kusikiliza na kuamua shauri hilo.

Katika uamuzi ulioandikwa na Jaji Issa Maige kwa niaba ya majaji wenzake waliosikiliza rufaa hiyo, Rehema Mkuye (kiongozi wa jopo) na Paul Kihwelo, Mahakama imeamuru kesi hiyo isikilizwe upya na Mahakama Kuu katika hatua ya pingamizi kwa mujibu wa sheria.

“Tumebaini rufaa hii ina mashiko, kitendo kilichofanywa na jopo la majaji watatu cha kumpangia jaji mmoja kusikiliza na kuamua pingamizi la awali kilikuwa kinyume cha mamlaka yao ya kisheria,” inaeleza sehemu ya hukumu ya Mahakama ya Rufaa.

Jopo hilo la majaji linaeleza: “Tunabatilisha na kufuta uamuzi na mwenendo mzima wa jaji mmoja. ‎Tunairidhia rufaa hii na tunaamuru pingamizi la awali lisikilizwe upya mbele ya Mahakama yenye mamlaka halali ya kusikiliza shauri hilo.”

Awali, wakili Mpoki alifungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu Masjala Kuu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. 

Katika kesi hiyo namba 25 ya mwaka 2019, Mpoki alikuwa akipinga baadhi ya vifungu vya Sheria ya Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, Sura 307 (TLS Act) kama ilivyofanyiwa marekebisho na Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 ya Mwaka 2018.

Vilevile, alikuwa akipinga Sheria ya Mwanasheria Mkuu (Utendaji wa Majukumu), Sura 268 (AG Act) kama ilivyorekebishwa na sheria hiyohiyo ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali.

‎‎Alilalamikia vifungu vya 15(3), 15A(1), (2) na 31(1) vya Sheria ya TLS , pia vifungu vya 5(2), (3), (6) na 27(3) na (5) vya Sheria ya AG.

Alidai vifungu hivyo vinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (kama ambavyo imekuwa ikifanyiwa marekebisho mara kwa mara, hususani Ibara za 13(1), 13(2), 13(6)(a), 20(1) hadi (4); 21(1) hadi (2) na 29(1).

Mpoki aliiomba Mahakama ivitangaze vifungu hivyo kuwa ni batili na iamuru viondolewe katika sheria hizo.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika majibu yake ya maandishi alipinga madai ya mdai, huku akiibua pingamizi la awali dhidi ya kesi hiyo kwamba, haistahili kusikilizwa akibainisha sababu sita. Pingamizi hilo lilisikilizwa na Jaji Benhajj Masoud.

Katika sababu ya kwanza ambayo ilikuwa msingi wa uamuzi, mdaiwa (AG) alidai  Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwani ilikwisha kuiamua.

Alifafanua kuwa awali kulikuwa na kesi ya aina hiyo namba 34 ya mwaka 2018 iliyofunguliwa na mlalamikaji huyohuyo dhidi ya mlalamikiwa huyohuyo iliyohusu madai hayohayo, ambayo ilitupiliwa mbali.

‎Jaji Masoud katika uamuzi alioutoa Aprili 30, 2020 aliitupilia mbali kesi hiyo ya pili, baada ya kukubaliana na sababu hiyo ya pingamizi la AG kuwa haikuwa na mamlaka kwani ilishakamilisha jukumu lake.

‎Mlalamikaji (wakili Mpoki) hakuridhika na uamuzi huo wa Mahakama Kuu, akakata rufaa akiwasilisha sababu nne za kuikata.

Mahakama ya Rufaa katika uamuzi wake imezingatia sababu moja ya rufaa kuwa jaji mmoja aliyeamua pingamizi hilo (Masoud), hakuwa na mamlaka hayo.

‎Wakati wa usikilizwaji wa rufaa, wakili wa mlalamikaji, Daimu Halfani, katika sababu hiyo alidai kesi ya awali ilipangwa kusikilizwa na majaji watatu ambao baadaye walimpangia jaji mmoja kusikiliza pingamizi la awali, kinyume cha sheria.

Aliirejesha Mahakama katika uamuzi wake kwenye kesi ya Onesmo Olengurumwa dhidi ya AG ya mwaka 2024 na akaiomba Mahakama iikubali rufaa hiyo.

‎Mjibu rufaa kupitia Wakili wa Serikali Mkuu, Hangi Chang’a alikiri kuwa jopo la majaji hao kumpangia jaji mmoja kusikiliza pingamizi hilo ilikuwa kinyume cha sheria.

Alieleza marekebisho katika kifungu cha 10 cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi na Wajibu, Sura 3 (Bradea), kupitia Sheria namba 2 ya 2025 ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, sasa mashauri chini ya sheria hiyo husikilizwa na majaji watatu katika hatua zote.

Hata hivyo, aliiomba Mahakama iitupilie mbali rufaa hiyo kwa madai kuwa dosari hizo za kiutaratibu haziathiri haki ya upande wowote, hivyo si sahihi kuamuru isikilizwe upya, huku akiirejesha Mahakama katika uamuzi wa kesi mbalimbali ilizowahi kuziamua.

‎Akijibu hoja hiyo, wakili Halfani alieleza Kanuni ya 7(2) ya Kanuni za Sheria ya Bradea GN (Tangazo la Serikali) namba 304/2014, ilimpa jaji mmoja mamlaka ya kusikiliza pingamizi kwa kupangiwa na Jaji Mfawidhi, si jopo la majaji.

‎Mahakama katika uamuzi imesema kabla ya marekebisho ya mwaka 2025, mashauri ya Kikatiba yalikuwa yanasimamiwa na Sheria ya Bradea, kifungu cha 10(1) pamoja na Kanuni zake GN namba 304/2014.

Mahakama imesema kwa mujibu wa kifungu cha 10(1) cha Bradea, mashauri chini ya kifungu cha 9 cha sheria hiyo yalisikilizwa na majaji watatu katika hatua ya mwisho.

Imesema kanuni ya 7(2), ilitoa mamlaka kwa jaji mmoja kusikiliza mashauri hayo katika hatua ya pingamizi, lakini marekebisho ya mwaka 2025, sasa mashauri hayo husikilizwa na majaji watatu hata katika hatua hiyo.

Hivyo, imesema kwa kuwa katika rufaa hiyo pingamizi la awali liliamuliwa Aprili 30, 2020, kabla ya marekebisho hayo jaji mmoja alikuwa na mamlaka ya kuamua shauri katika hatua ya pingamizi.

Mahakama imebainisha kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 15(1) Jaji Mfawidhi wa Kanda ndiye alikuwa na mamlaka ya kumpangia jaji mmoja kusikiliza kesi katika hatua ya pingamizi la awali.

‎Hata hivyo, imesema katika rufaa hiyo, jaji mmoja aliyesikiliza pingamizi hilo alipangiwa na jopo la majaji watatu lililoongozwa na Jaji Mfawidhi, mamlaka ambayo halikuwa nayo badala ya jaji mfawidhi mwenyewe.

‎”Hivyo, jaji aliyesikiliza hoja za awali hakuwa na mamlaka ya kisheria ya kuzisikiliza,” imesema Mahakama ya Rufaa katika uamuzi wake na kwamba, dosari hiyo inakwenda kwenye kiini cha kesi na kuhitimisha.

“Kwa hiyo, hatua sahihi kwa Mahakama ni kufuta mwenendo mzima na uamuzi wa Mahakama Kuu na kuamuru hoja hizo za pingamizi zisikilizwe upya kwa mujibu wa sheria,” imeamuru mahakama hiyo.