TMA YAKUSANYA KIJIJI NANENANE YATOA ELIMU KWA JAMII

::::::::

Na Mwandishi Wetu 

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetumia fursa ya Maonesho NaneNane 2025 Kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni, Dodoma kutoa elimu kwa jamii kuhusu huduma zitolewazo pamoja na jukumu kubwa la TMA la kudhibiti shughuli za hali ya hewa nchini.

Kupitia maonesho haya, wananchi na wadau mbalimbali wakiwemo wakulima, wavuvi na wafugaji wamepata elimu ya moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wa TMA wakiwemo viongozi.

TMA imeeleza namna taarifa za hali ya hewa zinavyokusanywa, kuchakatwa na kuchambuliwa kupitia mifumo ya kisasa, na jinsi huduma hizo zinavyoweza kusaidia jamii.Aidha, TMA imeeleza umuhimu wa kuendesha shughuli za hali ya hewa zenye kukidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA ,Dkt.Ladislaus Chang’a na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), akiwahudumia wateja kwenye Banda la Mamlaka aliwahimiza wadau wote kufuatilia utabiri wa kila siku, utabiri wa msimu pamoja na tahadhari za hali mbaya ya hewa, huku akisisitiza matumizi sahihi ya taarifa hizo katika shughuli zote za kiuchumi na kijamii.

Aidha, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya hali ya hewa na rasilimali watu na hivyo kuleta maendeleo makubwa ya utendaji kazi wa Mamlaka.

Mamlaka ya Hali ya HewaTanzania inashiriki katika maonesho ya NaneNane Dodoma, Zanzibar, Mbeya na Morogoro.Kauli Mbiu ya mwaka huu ni “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025”.