Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) leo kinatarajiwa kutangaza matokeo ya kura za maoni za wagombea ubunge katika majimbo mbalimbali nchini, hatua muhimu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Aliyekuwa Mbunge wa Pangani, Mkoa wa Tanga, Jumaa Aweso ameongoza kwenye kura za maoni kwa kupata asilimia 100 ya kura zote 3,806 zilizopigwa katika kata 14 za jimbo hilo.
Akizungumza na Mwananchi, kuhusu matokeo hayo leo Jumatatu Agosti 4, 2025 Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Pangani, Abdul Swala amesema katika kata zote za jimbo hilo Aweso ameongoza kwa kura huku wagombea wenzake wakipata sifuri, hivyo kuibuka mshindi.
Mbali na Aweso, wengine ni Mariam Abdallah na Ramadhan Zuberi.
Amesema katika uchaguzi huo wajumbe wote ni 3,843 ambao walitakiwa kupiga kura, lakini 37 hawakufika kwenye vituo vya kupigia kura na kufanya jumla ya kura zilizopigwa kuwa 3,806 ambapo hakuna iliyoharibika.
Baada ya matokeo hayo, Aweso anayetetea jimbo hilo kwa kipindi cha tatu ambaye pia ni Waziri wa Maji ametumia ukurasa wake wa kijamii wa Instagram kushukuru kwa kuandika: Asanteni sana wajumbe wa CCM Jimbo la Pangani kwa kura zote za ndio. Imani hii mlionipa nitailipa kwa matendo.”
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Bukombe,Dk Dotto Biteko ameibuka mshindi wa kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kupata asilimia 99.8 ya kura zilizopigwa.
Akizungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu, Katibu wa CCM Jimbo la Bukombe, Mwakalukwa Leonard, amesema jumla ya wajumbe 7,456 walishiriki kupiga kura ambapo kura halali zilikuwa 7,441 huku kura 15 pekee zikiharibika.
“Kura zote 7,456 zilipigwa, hakuna kura ya hapana, kura 15 zimeharibika,”amesema
Biteko alikuwa mgombea pekee katika nafasi ya ubunge kwa Jimbo la Bukombe katika mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, ameongoza kura za maoni katika nafasi ya ubunge Jimbo la Arusha Mjini kwa kupata kura 9,056.
Makonda na wenzake sita walikuwa wakiwania nafasi kupeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi (CCM), katika jimbo hilo ambalo lilikuwa likiongozwa na Mrisho Gambo.
Matokeo hayo yametangazwa leo Jumatatu Agosti 4,2025 na Mkurugenzi wa uchaguzi ambaye pia ni Katibu wa CCM Wilaya ya Arusha, Timothy Sanga amesema jumla ya wajumbe ilikuwa ni 10,186 ila waliopiga kura ni 9,276.
Wengine na matokeo yao kwenye mabano ni Mustapha Nassoro (83),Hussein Gonga (46),Ally Babu (28),Aminatha Toure (26),Lwembo Mghweno (16) na Jasper Kishumbua (10).
Aliyekuwa mbunge wa Songea Mjini, Dk Damas Ndumbaro ameongoza kura za maoni katika nafasi ya ubunge Jimbo la Songea Mjini kwa kupata kura 3,391 kati ya kura 6,795 zilizopigwa.
Dk Ndumbaro na wenzake wanne, walikuwa wakiwania nafasi ya kupeperusha bendera ya CCM katika Jimbo la Songea Mjini kwenye uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025. Ndumbaru anatetea kiti hicho.
Akitangaza matokeo hayo leo, Mkurugenzi wa uchaguzi ambaye pia ni Katibu wa CCM Wilaya ya Songea, James Mgego amesema jimbo hilo lina jumla ya kata 21 kura halali zilizopigwa ni 6,736 na zilizoharibika ni 59.
Amemtaja aliyeshika nafasi ya pili ni Hemed Challe aliyepata kura 2,839, Amandus Tembo kura 279, Issa Mkwawa kura 143 na Regan Mbawala kura 84.
Hata hivyo, msimamizi huyo amesema kura zilizopigwa leo ni za maoni, mchakato bado unaendelea. “Kwa hiyo wagombea wote muendelee kuwa watulivu kama tulivyofanya leo, uchaguzi umekuwa wa haki na amani imetawala,” amesema Mgego.
(Imeandikwa na Joyce Joliga).
Aliyekuwa mbunge wa Missenyi mkoani Kagera, Florente Kyombo ameongoza kura za maoni kwa kupata kura 2,979 kati ya 5,919 zilizopigwa katika vituo 22 za jimbo hilo.
Msimamizi wa uchaguzi wa Chama cha mapinduzi (CCM), Bakari Mwacha amesema kati ya wajumbe 5,919 waliotakiwa kupiga kura, 5,124 ndiyo walipiga kwenye vituo vyote.
Mwacha amemtaja Kyombo anayeomba ridhaa ya kutetea nafasi hiyo kwa kupata kura 2,979 akifuatiwa na aliyekuwa mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya, Projestus Tegamaisho aliyepata 1,355.
Wengine na kura zao kwenye mabano ni, Assumpter Mshama (475), Pelacius Ndibalema (166), Naswiru Byabatokura (88), Jacklyne Rushaigo (52), Jacklyne Rushaigo (52) na Amina Athuman kura tisa.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa matokeo zaidi