Msuva: Stars itavunja rekodi CHAN

NYOTA wa Al-Talaba SC ya Iraq, Simon Msuva ameweka wazi matumaini yake kwa Taifa Stars, huku akisisitiza huu ndiyo wakati wa kuvunja rekodi zote mbovu na kutinga fainali ya Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) ikiwa ni kwa mara ya tatu kushiriki mashindano hayo.

Akiwa na historia ndefu ya kuitumikia timu ya taifa na uzoefu mkubwa wa soka la kimataifa, Msuva alisema anachokiona kwa sasa Stars si kikosi cha wachezaji wenye uwezo wa kufanya makubwa.

“Ushindi dhidi ya Burkina Faso ni mwanzo mzuri, lakini pia ni ujumbe kuwa wachezaji wetu wamekomaa, wanacheza kwa akili na moyo ya kupambania nchi. Tukiendelea hivi, si ajabu tukaingia fainali,” alisema Msuva.

Stars ipo Kundi B pamoja na Madagascar, Mauritania, Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati, ikiwa ni sehemu ya mataifa matatu yaliyopewa heshima ya kuandaa CHAN kwa mara ya kwanza sambamba na Kenya na Uganda.

Msuva alisema kuwa wenyeji ni fursa ambayo haitakiwi kupuuzwa kwani mazingira ya nyumbani yanatoa motisha ya ziada kwa wachezaji kufanya makubwa.

“Tupo nyumbani, tuna sapoti ya mashabiki, mazingira tunayajua vizuri. Tunachotakiwa kufanya ni kutumia fursa hii kwa makini. Hatuhitaji miujiza, tunahitaji nidhamu, umoja na mpango wa kweli wa kiufundi. Nafasi ipo, rekodi mpya inawezekana,” alisema.

Kwa miaka ya nyuma, Stars imeshiriki CHAN mara mbili tu mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2009 Ivory Coast na ilipangwa kundi A pamoja na Senegal, Zambia na wenyeji.

Stars ilianza kwa kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Senegal katika mechi ya ufunguzi iliyopigwa Februari 22, 2009 na ikaondolewa mapema bila kushinda mchezo wowote. Michuano hiyo ilimalizika kwa DR Congo kutwaa taji la kwanza baada ya kuifunga Ghana 2-0 kwenye fainali.

Baada ya miaka 11, Tanzania ilirudi tena CHAN mwaka 2020 katika fainali zilizofanyika Cameroon. Stars ilipangwa kundi D pamoja na Guinea, Zambia na Namibia. Mechi ya kwanza ilichezwa Januari 19, 2021 na Stars ilianza tena kwa kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Zambia.

Baadaye ilishinda dhidi ya Namibia na kutoka sare na Guinea, lakini pointi nne hazikutosha kuivusha hatua ya makundi. Guinea na Zambia waliongoza kundi kwa pointi tano kila mmoja, huku Tanzania ikimaliza nafasi ya tatu.