The Cranes yaanza kwa fedheha CHAN 2024

TIMU ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’ imeanza vibaya Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), baada ya kuchapwa mabao 3-0 na Algeria katika pambano la kwanza la ufunguzi.

Katika mechi hiyo ya kundi C iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini Kampala, Algeria ilianza kupata bao la kwanza dakika ya 36 lililofungwa na nahodha Ayoub Ghezala aliyeunganisha mpira wa kona kwa kichwa uliopigwa na Abderrahmane Meziane.

Licha ya wenyeji kucheza soka safi na kutengeneza mashambuliaji mbalimbali, lakini Algeria waliongeza bao la pili dakika ya 76 lililofungwa na Abderrahmane Meziane aliyepiga shuti kali na kumshinda kipa wa Uganda, Jude Ssemugabi.

Bao la tatu la Algeria lililopoteza matumaini kwa wenyeji kuchomoa  limefungwa na Soufiane Bayazid dakika ya 79 ikiwa ni muda mfupi tangu nyota huyo aingie dakika ya 69 akichukua nafasi ya Aimen Mahious.



Kwa matokeo hayo Algeria inaongoza kundi C na pointi tatu sawa na Guinea iliyo nafasi ya pili baada ya kuanza vyema kwa kuichapa Niger bao 1-0, huku Afrika Kusini ikishika nafasi ya tatu wakati Uganda inaburuza mkiani mwa kundi hilo.

Matokeo hayo yanaifanya Uganda kuwa timu pekee mwenyeji wa CHAN 2024 kuanza kwa kichapo baada ya Taifa Stars kushinda mechi ya kwanza kwa mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Agosti 2, 2025.

Wenyeji wengine wa michuano hiyo, timu ya Taifa ya Kenya ‘Harambee Stars’ iliyo kundi A ilianza pia vyema jana baada ya kuifunga DR Congo bao 1-0 lililofungwa na Austine Odhiambo aliyepokea pasi ya David Sakwa.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Uganda ndilo taifa lililofanikiwa zaidi kutoka ukanda wa CECAFA likiwa na mataji 40, huku likishiriki CHAN mara ya saba baada ya kufanya hivyo 2011, 2014, 2016, 2018, 2020, 2022 na 2024.



Uganda imeendeleza rekodi mbovu kwa Algeria kwani kabla ya pambano la leo mara ya mwisho kukutana kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ambapo The Cranes ilichapwa mechi zote.

Katika mechi ya kwanza Algeria ilishinda nyumbani mabao 2-0, Juni 4, 2022, huku ile ya marudiano iliyopigwa Uganda kikosi hicho kikashindwa kutamba mbele ya mashabiki wake baada ya kukubali kupoteza tkwa mabao 2-1, Juni 18, 2023.

Kwenye kundi hilo, Algeria ilikuwa vinara na pointi 16 ikifuatiwa na Tanzania iliyomaliza ya pili na pointi nane, huku Uganda ikiwa ya tatu na pointi saba wakati Niger iliburuza mkia baada ya timu hiyo kuambulia pointi mbili.

Hata hivyo, katika fainali za CHAN zilizofanyika Sudan mwaka 2011, timu hizo zilipangwa kundi moja la A, ambapo Uganda ilichapwa tena mabao 2-0, yaliyofungwa na Abdelmoumene Djabou na Hillal Soudani, mechi iliyopigwa Februari 5, 2011.

Katika fainali hizo zilizoshuhudia Tunisia ikitwaa ubingwa wenyeji Sudan wakimaliza vinara wa kundi A na pointi saba, Algeria ikishika ya pili na pointi tano, huku Gabon ikimaliza ya tatu na pointi nne, wakati Uganda ilichapwa mechi zote.