Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya kusafirisha kilo 332 za dawa za kulevya aina ya heroini na methamphetamine inayomkabili mvuvi Ally Ally (28), maarufu Kabaisa na wenzake wanane umekamilika, mahakama imeelezwa.
Wakili wa Serikali, Pancrasia Protas, ameeleza hayo leo Agosti 4, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, shauri hilo lilipotajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga.
Usikilizwaji umefanyika kwa njia ya video washtakiwa wakiwa mahabusu.
Mbali na Kabaisa, washtakiwa wengine ni mfanyabiashara Bilal Hafidhi (31), mvuvi, Mohamed Khamis (47) na muuza magari, Idrisa Mbona (33).
Wengine ni Rashid Rashid (24), mkazi wa Ubungo Maji, Shabega Shabega (24), mbeba mizigo na mkazi wa Saadan Kasulu, mlinzi na mkazi wa Madale Kisauke, Dunia Mkambilah (52), mfanyabiashara mkazi wa Mwambani, Mussa Husein (35) na Hamis Omary (25).
“Kesi imeitwa kwa ajili ya kutajwa, naomba kuitaarifu mahakama kuwa upelelezi wa shauri hili umekamilika na tumeshawasilisha taarifa na nyaraka muhimu Mahakama Kuu kwa ajili ya kusajiliwa, hivyo kutokana na taarifa hii, tunaomba mahakama itupangie tarehe kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo nyaraka hizo zimeshasajiliwa ili tuendelee na hatua nyingine,” amesema wakili huyo.
Hakimu Mwankuga amekubali ombi hilo na kuahirisha shauri hilo hadi Agosti 18, 2025 kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo nyaraka hizo zimeshasajiliwa.
Washtakiwa wapo rumande kutokana na kesi inayowakabili kutokuwa na dhamana.
Katika shauri hilo, washtakiwa wanadaiwa Aprili 16, 2024 karibu na Hoteli ya White Sands, iliyopo wilayani Ilala, walikutwa wakisafirisha kilo 100.83 za dawa za kulevya aina ya methamphetamine, kinyume cha sheria.
Shtaka la pili, wanadaiwa siku na eneo hilo, kwa pamoja walisafirisha kilo 232.69 za heroini kinyume cha sheria.
Walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Aprili 22, 2024 na kusomewa mashtaka hayo.