Beki Yanga amlilia Jonathan Sowah

MSHAMBULIAJI mpya wa Simba, Jonathan Sowah ameshaanza mazoezi akiwa na kikosi cha timu hiyo kilichopo Misri, lakini kuna beki mmoja aliyewahi kukipiga Yanga ameshtushwa na kuumizwa juu ya kutua huko badala ya Jangwani na kusema timu hiyo isipojipanga ijue mapema itaumia kwake.

Joseph Zutah aliyeitumikia Yanga kwa muda mfupi ambaye sasa ni bosi pale Medeama ya Ghana ameliambia Mwanaspoti, alikuwa anafahamu kwa kina kwamba tangu timu yake hiyo ilipokutana na Sowah misimu miwili iliyopita, mabingwa hao wa soka Tanzania walikuwa wakitaka kumsajili.

Zutah alisema kila wakati alipokuwa anazungumza na Sowah, alikuwa anapata taarifa njema kwamba atakwenda Yanga, lakini ghafla mambo yamegeuka na kusajiliwa Simba.

Beki huyo aliongeza, Yanga kumkosa Sowah sio taarifa nzuri kwa mashabiki wa timu hiyo, ambapo watatakiwa kujipanga kuzima kasi yake kutokana na ubora alionao mshambuliaji huyo wa zamani wa Singida Black Stars.

“Unajua tangu tulipokutana na Yanga (Medeama) nilikuwa naongea na viongozi wa Yanga kwamba wanamtaka Sowah na hata mchezaji mwenyewe alikuwa akinijulisha taarifa nzuri kwamba anatamani kucheza pale,” alisema Zutah ambaye alisajiliwa Yanga na kocha Hans Pluijm.

“Wiki iliyopita nilishtuka kuona kwamba Sowah anakwenda Simba, sikuamini, nilimtafuta Sowah akaniambia kweli anahamia Simba, iliniumiza sana. Niseme ukweli, Yanga wamepoteza nafasi ya kuwa na mshambuliaji mzuri mwenye ushindani,” alifafanua Zutah na kuongeza;

“Sowah sio mchezaji mkorofi ni mchezaji mshindani, hata tulipokuwa naye hapa alikuwa hataki kuona timu yake inapoteza kirahisi hata kwenye mazoezi.

“Ni mshambuliaji ambaye hajui kuogopa kupambana kufunga mbele ya beki yeyote sasa ile hali ndio watu wanaona mkorofi, nadhani Simba imepata mshambuliaji wa daraja kubwa anayejua kufunga.”

Yanga ilitajwa ilikuwa mbioni kumnasa straika huyo aliyesajiliwa dirisha dogo la msimu uliopita na kuitumikia Singida BS katika mechi 14 na kuifungia mabao 13.