MABOSI wa JKT Tanzania wamedaiwa kuweka ngumu kumruhusu kipa wa timu hiyo, Yakoub Suleiman kujiunga na Simba iliyopiga kambi Misri ikijiandaa na msimu mpya wa 2025-2026, hivyo kuwafanya wenzao wa Msimbazi kulazimika kuongeza dau ili kuhakikisha wanamnasa mapema.
Tangu dirisha la usajili lilipofunguliwa, Simba ilikuwa inatajwa kumwania kipa huyo ambaye ni kipa namba moja wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayoshiriki michuano ya CHAN 2024, akitajwa kama mtu sahihi wa kumpa changamoto kipa wa sasa Moussa Camara baada ya Aishi Manula kuondoka kujiunga na Azam kutokana na kumaliza mkataba aliokuwa nao Msimbazi.
Kocha wa Simba, Fadlu Davids ndiye anayesimamia usajili wa timu hiyo na alishawaeleza mabosi wa timu hiyo kuwa wapambane kadri wanavyoweza kumsajili kipa huyo.
Yakoub ambaye ni muajiriwa wa Jeshi la Kujenga Uchumi la Zanzibar (JKU), amekutana na kigingi kikubwa baada ya kudaiwa, timu yake inataka kitita kikubwa ili kumuachia jambo ambalo linaonekana kuzifanya timu nyingi kurudi nyuma katika dili hilo, lakini ikielezwa sasa inapelekwa ofa nyingine ya mwisho.
Chanzo cha ndani kilisema, wachezaji askari wanaotoka Zanzibar wanaweza wakacheza timu yoyote Bara kwa makubaliano maalumu na waajiri wao, kama ilivyo kwa Ibrahim Hamad ‘Bacca’ wa Yanga ambaye bado ni askari wa jeshi la KMKM.
“Yakoub ni askari wa JKU ya Zanzibar kwa takribani miaka mitano, hivyo anaposajiliwa na timu yoyote pesa yake ya usajili anagawana na waajiri wake kati kwa kati bila kujali anacheza timu ya jeshi au la,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Mfano huyo Yakoub pamoja na kucheza JKT Tanzania ambayo pia ni timu ya jeshi, lakini bado anapokea mshahara kazini kwake JKU kila mwezi mbali na ule anaoupata katika timu.”
Yanga ndio ilikuwa ya kwanza kusaka huduma ya Yakoub, ilitaka kumpa Sh100 milioni kwa mkataba wa miaka mitatu, maslahi ambayo kwa upande wa mchezaji hakuona kama yanamfaa.
“Yanga ilimtaka Yakoub baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu msimu ulioisha wakati huo alikuwa na mkataba wa miezi sita, lakini kutokana na kipengele cha ajira yake, angechukua Sh100 milioni angebakiwa na Sh50 milioni kwa miaka mitatu, jambo ambalo kwake aliona halina maslahi,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Baada ya kuona imeshindikana kwa Yanga mchezaji huyo aliongeza mkataba wa miaka miwili na JKT Tanzania, hivyo Simba itatakiwa iununue mkataba huo ili ajiunge nao ambapo JKT nayo kwa sasa inataka kitita kikubwa cha fedha.”
“Kuna sehemu watu wanachanganya, wakati ofa ya kwanza inakwenda kwa Yakub alikuwa anaweza kusaini kama mchezaji huru, lakini sasa ana mkataba mpya na JKT ambao kwa kweli ni fedha nyingi wamempa, hivyo kama Simba ni kweli kwamba wanapeleka ofa ya milioni 180, JKT hawawezi kukubali, lakini kumbuka kuwa lazima mchezaji naye atakuwa ana kiwango anachotakiwa kupewa.”
“Tusubiri tuone lakini naamini ofa hiyo inaweza kwenda klabuni ndani ya wiki hii, sidhani kama dili litafanikishwa kwa kiwango hicho cha fedha isipokuwa kama watajipiga vizuri, lakini ukweli huyu ni mmoja kati ya makipa bora nchini kwa sasa.”
Msimu uliopita JKT ilimaliza Ligi katika nafasi ya sita, huku Yakoub ndiye aliyekuwa kipa namba moja wa timu hiyo na iliruhusu mabao 27 tu katika michezo 30 ya Ligi, akiwa ndiye kipa mzawa ambaye aliruhusu mabao machache, lakini kwa ujumla akishika nafasi ya tano nyuma ya wale wa Yanga, Simba, Singida Black Stars na Azam.