TBS YAIPONGEZWA KWA KULINDA UBORA NA AFYA ZA WALAJI, YATAKIWA KUONGEZA NGUVU ZA USIMAMIZI

Farida Mangube, Morogoro

Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Mussa Ali Mussa, ameipongeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa kazi kubwa inayofanya katika kulinda ubora wa bidhaa na afya za walaji nchini, huku akilitaka shirika hilo kuongeza juhudi zaidi katika kusimamia ubora wa bidhaa zinazozalishwa na kuingia sokoni.

Dkt. Mussa ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la TBS katika Maonesho ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nanenane) Kanda ya Mashariki yanayoendelea katika Viwanja vya Nanenane, mkoani Morogoro, ambapo alipata fursa ya kuona shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na shirika hilo.

“Nawapongeza kwa kazi nzuri ya kulinda ubora wa bidhaa. Afya za wananchi zinategemea sana kazi mnayofanya. Ni muhimu kuendelea kuongeza nguvu, hasa katika kipindi hiki ambacho kuna ongezeko kubwa la bidhaa mbalimbali sokoni alisema Dkt. Mussa.

Bw. Sileja Lushibika ni Afisa Mdhibiti Ubora kutoka TBS Kanda ya Mashariki, amesema kuwa TBS inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi mkubwa, ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa bidhaa, kutoa elimu kwa wazalishaji na walaji, kuthibitisha viwango, pamoja na kutoa alama ya ubora kwa bidhaa zinazokidhi viwango.

“TBS tunahakikisha bidhaa zinazoingia sokoni ni salama kwa matumizi ya binadamu na zinakidhi viwango vya ubora vilivyowekwa. Tunaendelea na ukaguzi katika viwanda, maduka, mipakani, pamoja na kutoa mafunzo kwa wazalishaji wadogo na wa kati kuhusu uzingatiaji wa viwango,” alisema Bw. Lushibika.

Aidha, Bw. Lushibika ametoa wito kwa wananchi wote kutembelea banda la TBS ili kujifunza kuhusu haki zao kama walaji, pamoja na wajibu wao katika kuhakikisha bidhaa wanazonunua ni salama na zenye ubora unaostahili.

“Wananchi mnakaribishwa banda la TBS. Elimu tunayotoa ni muhimu kwa kila mmoja, iwe ni mfanyabiashara, mkulima, mjasiriamali au mtumiaji wa kawaida. Kupitia elimu hii, tunaweza kwa pamoja kuimarisha afya za walaji na kukuza uchumi wetu kupitia bidhaa bora,” alihimiza.