Dar es Salaam. Mtandao wa Billionaires.Africa umetangaza orodha ya watu 10 matajiri zaidi nchini Tanzania, ukionyesha mchango wao katika uchumi wa Taifa kupitia uwekezaji katika sekta mbalimbali kama viwanda, mafuta, mawasiliano, na fedha.
Kinara wa orodha hiyo ni Mohammed Dewji, bilionea pekee wa Afrika Mashariki mwenye utajiri wa Dola bilioni 2.2 (Sh5.5 trilioni) kupitia kampuni yake MeTL Group. Anafuatiwa na Rostam Aziz, aliyewahi kuwa mbia mkubwa wa Vodacom Tanzania na sasa anawekeza kwenye gesi na madini, akiwa na utajiri wa Dola 700 milioni (Sh1.75 trilioni).
Wengine kwenye orodha hiyo ni Said Salim Bakhresa wa Bakhresa Group Dola 400 milioni (Sh1.04 trilioni) , Ally Awadh wa Lake Oil Dola 180 milioni (Sh450 bilioni), Edha Nahdi, Mkurugenzi Mtendaji wa Amsons Group anayekadiriwa kuwa na utajiri wa dola 120 millioni (Sh300 bilioni).
Wengine ni Seif Ali Seif Dola 90 milioni (Sh225 bilioni), mfanyabiashara huyu ni mwanzilishi wa Super Group. Ingawa hana mazoea ya kujitokeza hadharani, ana ushawishi mkubwa katika sekta za sukari, usafirishaji na viwanda.
Anayefata ni aliyekuwa mwanzilishi na mshirika mkuu wa Precision Air Services, Michael Shirima aliyekadiriwa kuwa na utajiri wa dola 45 milioni (Sh112 bilioni). Mungine ni Ketan Patel, mfanyabiashara maarufu wa dhahabu ana utajiri wa dola 25 milioni (Sh62 bilioni).
Wengine ni Patrick Schegg, mwenye utajiri wa Dola 20 milioni (Sh50 bilioni) ni mwekezaji mashuhuri katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na alikuwa meneja wa mfuko wa uwekezaji wa kimataifa na Hans Aingaya Macha akiwa na utajiri wa Dola 15 milioni (Sh37 bilioni) ni miongoni mwa wawekezaji tajiri zaidi nchini Tanzania na ana mchango mkubwa katika shughuli za Soko la Hisa la DSE.