Simba yafuata mwingine Congo | Mwanaspoti

KIKOSI cha Simba kinaendelea kujifua mazoezi kambini Ismailia, Misri, huku mabosi wakiendelea kupiga hesabu kushusha mashine za mwishomwisho kwa msimu ujao, huku ikielezwa kwa sasa wamehamia kwa beki raia wa Kongo – Brazzaville.

Kikosi cha wababe hao kipo maandalizi makali mjini Ismailia ambako mastaa wa zamani na wapya wanajifua na kufuliwa vilivyo na benchi la ufundi chini ya Kocha Fadlu Davids aliyetoka kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara dakika za lalasalama msimu ulioisha.

Na sasa inaelezwa kwamba timu hiyo ipo katika hatua za mwisho kumsafirisha ili kumleta mjini beki wa kushoto, Hernest Malonga.

Malonga alitua Tanzania Januari 2024 katika dirisha dogo la usajili la 2023-2024 ili kujiunga na Ihefu (sasa Singida Black Stars), kisha kutolewa kwa mkopo Coastal Union na Tabora United kwa vipindi tofauti msimu uliopita.

Beki huyo ambaye alisaini mkataba wa miaka miwili uliomalizika msimu uliopita kwa sasa ni mchezaji huru.

Mwanaspoti linafahamu kuwa, Simba iko katika mazungumzo na beki huyo ili aongeze nguvu eneo la ulinzi la kushoto  lililoondokewa na mabeki Mohammed Hussein na Valentin Nouma.

Taarifa za ndani zimelidokeza gazeti hili kwamba, mabosi hao wana mpango wa kumleta Malonga Dar kisha kumsafirisha hadi Misri ili kocha aangalie kama kiwango chake kitamfaa kama ilivyo kwa wachezaji wengine waliopo kambini wakifanyiwa majaribio na benchi la ufundi.

“Ujue bado tunaendelea kusajili – kwenda pre season sio sababu ya kuacha kuongeza wachezaji, ila Malonga akifika mipango yetu ni kwamba aonane na kocha ili aweze kumuangalia. Kuna mawili – akaenda Misri au wakakutana baada ya kurudi. Lengo ni kuwa na wachezaji wasiopungua wawili hadi watatu katika kila eneo uwanjani,” chanzo kilidai.

Kuhusu idadi ya wachezaji wa kigeni, taarifa zinadai kwenda kambi Misri haina maana wapo katika mipango ya timu, kwani bado kocha Fadlu Davids yupo kwenye mchujo wa kuangalia nani abaki na yupi aondoke.

“Watakaporudi wapo watakaoenda kwa mkopo timu zingine na watakaosalia kutokana na viwango ambavyo watavionyesha huko Misri. Kwa hiyo chekeche bado halijaisha.”

Ikumbukwe kuwa Simba imekwishafikisha idadi ya wachezaji wa kigeni ambao wanahitakiwa kikanuni (12), hivyo huenda itampunguza mchezaji ili kumuingiza Mkongomani huyo iwapo atalivutia benchi la ufundi.

Simba ilishawahi kuwakata wachezaji waliokuwa kambini akiwamo Meddie Kagere misimu miwili iliyopita. Wiki iliyopita  iliondoka na baadhi ya wachezaji kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao.