Imekuwa kama fasheni flani iliyoibuka hivi karibuni hapa nchini kwa watu kutembelea kwenye bustani za wanyama pori (zoo) wakiwemo wanyama hatari kama Simba na wengineo na kuwachezea au kuwalisha vyakula wakiwa nao.
Katika matukio hayo tumewashuhudia watu wakipiga picha kuwachezea simba na kuwalisha chakula wanyama kama vile twiga na ndege wakubwa kama vile, mbuni, korongo na wengineo.
Akizungumza na mwandishi wetu kwenye banda la Dar es Salaam Zoo lililopo kwenye Maonesho ya Nanenane, Morogoro Afisa Wanyama pori Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama pori nchini (TAWA) aliyejitambulisha kwa jina la Proches Rongoma, amesema vitendo vya kucheza na mnyama kama simba ni hatari mno. Aliendelea kusema;
“Mnyama wa porini ni mnyama wa porini, hata ukimlea tangu utotoni na kumfundisha kuishi na binadamu baadae mnyama huyo kadili anavyozidi kukua anaweza kubadilika kitabia na kuwa na tabia zake za asili kama awapo msituni na hivyo kuweza kufanya lolote na hata kuwadhuru wanaomfuga.
Hivyo nawatahadharisha wanaokwenda zoo kucheza na simba wanaofugwa wafanye hivyo kwa tahadhari kwasababu kuna ushahidi wa simba wa kufugwa waliowahi kuwabadilikia binaadamu kwenye zoo. Alimaliza kusema afisa huyo.