Morogoro. Wakulima wa mazao mbalimbali ya chakula na biashara wametakiwa kufuata kanuni bora za kilimo ikiwa ni pamoja na kupima afya ya udongo ili waweze kujua aina na kipimo cha mbolea kinachohitajika.
Wito huo umetolewa na Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya wilaya ya Gairo, Christopher Mussa wakati akizungumza na Mwananchi kuhusu mbolea aina ya Minjingu ambayo imekuwa ikitumiwa na wakulima wengi wilayani humo, baada ya kuonekana kufanya vizuri hasa kwenye mazao ya chakula na mbogamboga.
Amesema kabla ya kutumia mbolea yoyote wakulima wa wilayani humo wamekuwa wakishauriwa kupima afya ya udongo kwa kutumia kipimo ambacho kipo kwenye maabara ya halmashauri hiyo, ili kujua hali ya afya ya udongo na aina ya mbolea wanazoweza kuzitumia.
“Ni kweli mkulima akitumia mbolea bila ya kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa kilimo anaweza kupata hasara kwenye mazao yake na ndio maana halmashauri yetu iliamua kununua kipimo cha kupima afya ya udongo, (soil scanner), na kipo pale ofisi za halmashauri na wakulima wanapimiwa udongo kwenye mashamba yao bila gharama yoyote,” amesema Mussa.
Kwa upande wake, mmoja wa wakulima wanaotumia mbolea ya Minjingu, Anjela Josephat kutoka Mgeta wilaya ya Mvomero amesema tangu ameanza kutumia mbolea hiyo mazao yamekuwa yakiua bila changamoto yoyote.
“Mimi ni mkulima wa mbogamboga kama kabeji, karoti na pilipili hoho mwanzoni kabla sijaitumia hii mbolea nilikuwa siielewi lakini baada ya kuja kwenye banda hili mwaka jana na kupata elimu na baadaye kuanza kuitumia sasa nimeielewa na ninaiamini kwa kiasi kikubwa, mazao yangu yanakuwa vizuri,” amesema Josephat.
Ofisa Kilimo wa kampuni hiyo, Franks Kamhabwa amesema katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na changamoto mbalimbali za mabadiliko ya tabianchi wakulima wanapaswa kutumia mbolea ikiwa ni moja ya njia ya kukabiliana na mabadiliko hayo, ambayo yamekuwa pia yakiathiri uzalishaji wa mazao mbalimbali.
Kamhabwa amesema kampuni hiyo ya Minjingu imekuwa ikizalisha mbolea za kupandia na kukuzia ambazo zinaweza kutumiwa kwenye mazao mbalimbali yakiwemo mazao ya chakula, mazao ya biashara na hata mazao ya mbogamboga isipokuwa Ile ya jamii ya mikunde kunde ambayo yenyewe haihitaji mbolea ya kukuzia.
“Kabla ya kumuuzia mkulima mbolea tumekuwa na utaratibu wa kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea hii, elimu hiyo ni ya namna gani ya kuweka mbolea kwenye shamba, aina gani ya mbolea inavyoweza kufaa kwenye mazao ya mkulima, ni wakati gani mazao yanatakiwa kuwekwa mbolea na mambo mengine ya msingi,” amesema Kamhabwa.
Kamhabwa amesema kampuni imekuwa na wajibu huo wa kutoa elimu kwa sababu mbolea yoyote ukitumika vibaya inaweza isitoe matokeo anayotarajia mkulima na wakati mwingine inaweza ikamsababishia hasara mkulima.