Serikali yaainisha mbinu wakulima kuyafikia masoko ya kimataifa

Arusha. Katika kuhakikisha sekta ya kilimo nchini inazidi kukua na kukuza uchumi wa wakulima, Serikali imewapa mbinu wakulima juu ya uzalishaji wa mazao yenye kukabiliana na vikwazo vya masoko ya kimataifa.

Lengo kubwa la mpango huo, mbali na kuongeza mauzo ya mazao nje ya nchi, lakini pia ni kuhakikisha inaongeza kiwango cha uzalishaji nchini na kuinua uchumi wa wakulima.

Mtafiti wa maswala ya viuatilifu na visumbufu mimea, kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Gabriel Mganga amesema kuwa kikwazo kikubwa cha biashara ya usafirishaji wa mazao nje ya nchi ni vigezo.

Amesema kuwa kigezo kikubwa cha mazao au bidhaa kupokelewa katika masoko ya kimataifa, mbali na kukidhi mahitaji na matakwa lakini pia lazima iwe huru dhidi ya visumbufu mimea ikiwemo magonjwa, wadudu na vimelea ambavyo vinaweza kusababisha magonjwa.

“Kwa utafiti tuliofanya hivi karibuni tumegundua kuwa wakulima wengi nchini wanakosa sifa ya kusafirisha mazao yao nje ya nchi kutokana na kutozingatia masharti na vigezo vya masoko haya ya kimataifa” amesema Mganga wakati akizungumza na mwananchi katika maonyesho ya wakulima Nanenane kanda ya kaskazini.

Amesema kuwa kwa mkulima anayetaka kusafirisha mazao yake nje ya nchi, anatakiwa kwanza kujua mahitaji au matakwa ya bidhaa anayotaka kupeleka na sifa zake katika nchi husika.

“Akishapata hilo anatakiwa kuja TPHPA Kwa ajili ya kupata wataalamu wa kufanya ukaguzi wa shamba na vipimo vya mazao au mavuno yake yakiwa shambani, ili kupewa kibali cha kibali cha usafirishaji au kusaidiwa kama itagundulika kuna tatizo la visumbufu vyovyote.”

“Bila kufanya hivyo mkulima anaweza kupata hasara ya kusafirisha bidhaa ambayo haihitajiki au haijakidhi vigezo ikakataliwa, lakini pia anaweza kuhatarisha nchi katika soko la nchi hiyo kuwa si salama na ikafungiwa” amesema.

Aidha sekta hii ya kilimo inayochangia asilimia 30 ya pato la Taifa mauzo yake nje ya nchi yamezidi kupaa na kufikia Dola za Marekani bilioni 3.54 (sawa na Sh9.558 trilioni) katika mwaka wa fedha 2023/2024, kutoka Dola bilioni 2.3 (sawa na Sh6.21 trilioni) katika mwaka wa fedha 2022/23.

Hata hivyo Serikali imejiwekea malengo ya kuhakikisha hadi mwaka 2030 mauzo ya mazao nje ya nchi yanafikia kiasi cha dola za Marekani bilioni 5 (sawa na Sh3.5 trilioni).

“Malengo hayo yanaweza kufikiwa na kupitiliza endapo wakulima wetu na wafanyabiashara watazingatia kanuni bora za kilimo, maelekezo ya wataalamu hasa katika kukabiliana na visumbufu mimea na kuchangamkia zaidi masoko ya kimataifa” amesema mtaalamu wa kudhibiti visumbufu vya milipuko kutoka TPHPA, Gladman Mbukoi.

Amesema kuwa changamoto kubwa kwa wakulima ni visumbufu mimea hasa wa milipuko wakiwemo ndege aina ya kwelea na nzige ambao huvamia mashamba.

“Kikubwa wakulima waache mazoea ya kupiga dawa kila wanapoona udhaifu wowote katika mimea yao bali watoe taarifa haraka kwa wataalamu wa kilimo katika ngazi ya kata au halmashauri ili waone jinsi ya kutatua katika hatua za awali na kuokoa mazao” amesema.

Mmoja wa wakulima katika maonyesho hayo, Beatrice Laizer ameiomba Serikali kuendelea kuwa na vituo vya elimu ya kilimo kila mwanzo wa msimu wa mvua kuliko kutegemea elimu ya Nanenane pekee.