BASHUNGWA AMUAGIZA IGP KUDHIBITI WAHALIFU WANAOTUMIA MITANDAO KUVURUGA AMANI.

 


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillus Wambura, kuhakikisha Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama linaimarisha doria mtandaoni (online patrol) kwa lengo la kudhibiti baadhi ya wahalifu wanaotumia mitandao kuvuruga amani na utulivu wa nchi, pamoja na kukabiliana na uhalifu unaofanyika kwa njia ya mtandao.

Bashungwa ametoa agizo hilo leo, tarehe 6 Agosti 2025, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kituo kipya cha Polisi cha “Daraja B” kilichopo Sanya Juu, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha miundombinu ya majengo na vitendea kazi ndani ya Jeshi la Polisi.

“IGP, kwa sasa baadhi ya wahalifu wamehamia kwenye mitandao. Kama mnavyofanya doria za kawaida, vivyo hivyo tuimarishe doria mtandaoni ili kudhibiti wizi wa kifedha na wahalifu wanaolenga kuvuruga amani na utulivu wa nchi yetu kupitia mitandao,” amesisitiza Bashungwa.

Aidha, Waziri Bashungwa amelielekeza Jeshi la Polisi kuendelea kutekeleza maagizo mbalimbali ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, yanayohusu kupambana na uhalifu, udhibiti wa madereva wazembe, pamoja na kuondoa vyombo vya moto visivyokidhi viwango vinavyosababisha ajali barabarani.

Bashungwa amelitaka Jeshi la Polisi kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kubaini maeneo hatarishi katika barabara kuu ambazo zimekuwa zikiripotiwa kusababisha ajali mara kwa mara, ili yafanyiwe upembuzi yakinifu na kutengewa bajeti kwa ajili ya kutafutiwa suluhisho la kudumu.

Katika hatua nyingine, Bashungwa amelitaka Jeshi la Polisi kuendelea kushirikiana na madereva wa pikipiki (boda boda) kwa kukutana na viongozi wao katika ngazi ya wilaya na mikoa ili kuwapa elimu ya usalama barabarani na kuweka mikakati ya pamoja ya kupunguza ajali nchini.

Kadhalika, Bashungwa ameviagiza vyombo vyote vya usalama vilivyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuendelea kushirikiana katika kuimarisha amani, usalama na utulivu, hasa katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na baada ya uchaguzi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillus Wambura, ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kudumisha amani na utulivu, huku akiwatoa hofu Watanzania kwa kuwahakikishia kuwa nchi ipo salama na itaendelea kuwa salama.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema kuwa kituo cha Polisi cha Wilaya ya Siha kimejengwa kwa fedha za Serikali kupitia Jeshi la Polisi, kwa kushirikiana na michango ya wananchi wa wilaya hiyo.