Namungo FC yatua kwa Kocha Mkongomani

UONGOZI wa Namungo FC umefungua mazungumzo ya kumuajiri Mkongomani Guy Bukasa ili akiongoze kikosi hicho msimu ujao, ikiwa ni hatua nyingine baada ya mabosi kushindwa kufikia makubaliano ya kumrejesha Mzambia Hanour Janza.

Janza aliyeifundisha timu ya Taifa ya Taifa Stars kisha baadaye kuteuliwa kuwa mkurugenzi wa Ufundi wa ZESCO United ya kwao Zambia alikuwa akipigiwa hesabu za kurejea Namungo baada ya awali kuitumikia na kuondoka Desemba 7, 2022.

Taarifa ambazo Mwanaspoti limezipata zinaeleza kwamba Janza alitaka kiasi kikubwa cha fedha ili arudi kuchukua nafasi ya Juma Mgunda aliyeondoka baada ya msimu wa 2024-2025 kwisha, japo dili hilo limekwama na uongozi kumpigia hesabu Bukasa.

Mgunda aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali zikiwemo Coastal Union, Simba na Simba Queens, alijiunga rasmi na Namungo Oktoba 24, 2024, akichukua nafasi ya Mkurugenzi wa Programu za Soka la Vijana wa kikosi hicho Mkongomani Mwinyi Zahera.

Kwa msimu wa 2024-2025, Mgunda aliiwezesha Namungo kumaliza nafasi ya tisa katika Ligi Kuu Bara na pointi 35, baada ya kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’, kushinda mechi tisa, sare minane na kupoteza 13, kikifunga mabao 28 na kuruhusu 36.

Sasa baada ya Mgunda kuondoka na dili la Mzambia kukwama, mabosi wa Namungo wamefungua mazungumzo ya kumpata kocha huyo raia wa DR Congo, ambaye awali alitangaza rasmi Mei 14, 2025 kuachana na timu ya vijana ya nchi hiyo chini ya miaka 20.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman aliliambia Mwanaspoti kama kuna taarifa juu ya suala hilo watazitolea ufafanuzi kwa mashabiki wao na kwa sasa wanaendelea kusajili nyota wapya kwa ajili ya msimu ujao.

Hata hivyo, licha ya kauli hiyo, Mwanaspoti linatambua kipaumbele cha kwanza cha Namungo ni kumpata Bukasa ambaye amezifundisha pia AS Dauphins Noirs na AS Nyuki za DR Congo pamoja na Rayon Sports, Gasogi United na AS Kigali za Rwanda.

Bukasa aliyezaliwa Machi 26, 1987 akiwa ni muumini wa mfumo wa 4-2-3-1, amewahi pia kufundisha akademi ya AS Marsa ya Tunisia, jambo ambalo linaonyesha kocha huyo kijana ana uzoefu, huku akibobea zaidi katika soka la vijana.