Dar es Salaam. Katika jitihada za kusaidia watoto wanaozaliwa na matatizo ya moyo, kampuni ya East African Crude Oil Pipeline (EACOP) imetoa msaada wa Sh100 milioni kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kugharamia matibabu ya watoto zaidi ya 25 pamoja na ununuzi wa vifaatiba.
Msaada huo umetolewa leo Agosti 6, 2025 jijini Dar es Salaam na kupokewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dk Peter Kisenge.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo Kisenge ameishukuru EACOP kwa mchango wao, akieleza kuwa idadi ya watoto wanaozaliwa na matatizo ya moyo imekuwa ikiongezeka kwa kasi nchini huku familia nyingi zikiwa hazina uwezo kugharamia matibabu.
“Kwa kila watoto 100 wanaozaliwa, takriban wawili wanakuwa na matatizo ya moyo. Gharama za matibabu ni kubwa zinaanzia Sh8 milioni hadi Sh15 milioni kwa mtoto mmoja. Familia nyingi haziwezi kumudu ndiyo maana tunashukuru kwa msaada huu mkubwa kutoka EACOP,” amesema Kisenge.
Ameongeza kuwa Serikali kwa kawaida hufadhili asilimia 70 ya gharama hizo, huku asilimia 30 zikibaki mikononi mwa familia, jambo linaloilazimu taasisi hiyo kuomba msaada kutoka kwa wadau mbalimbali ili kusaidia watoto zaidi kupata huduma hiyo muhimu.

Kwa upande wake Meneja wa ECOP Tanzania, Jofley Mponda amesema msaada huo ni sehemu ya mpango wa kampuni hiyo kurudisha kwa jamii na kusaidia maeneo yenye uhitaji mkubwa.
“Tunaelewa ongezeko la watoto wanaozaliwa na magonjwa ya moyo ni changamoto kubwa. Tunaamini msaada huu utasaidia kurudisha furaha katika familia nyingi, kwani mtoto mmoja akipona familia nzima hupona,” amesema Mponda.
Ameongeza kuwa EACOP itaendelea kufuatilia athari ya msaada huo na kuangalia uwezekano wa kutoa misaada zaidi siku za usoni.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka JKCI, Naizihijwa Majani amesema changamoto ya watoto kuzaliwa na matatizo ya moyo imeendelea kuongezeka nchini, huku wengi wao wakiwa hawana bima ya afya.
“Tofauti na watu wazima, watoto wakigundulika mapema na kupata matibabu hupata nafuu na kuendeleza na maisha kama kawaida,” amesema Naizihijwa.
Huku akiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuongeza taasisi za kutoa huduma hizo kwani kwa sasa nchi nzima inategemea JKCI pekee.
Meneja wa uwezekano na uwajibikaji kwa jamii wa EACOP Tanzania, Clare Haule amesema msaada huo umetolewa baada ya kupokea ombi rasmi kutoka JKCI, na umeelekezwa katika mikoa minane inayopitiwa na bomba la mafuta.
Mpaka sasa watoto 159 tayari wamepatiwa matibabu kupitia mpango huu, huku lengo likiwa kuwasaidia watoto 300 kufika mwisho wa mwaka huu.