Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alisema ni wakati muafaka kwa waandishi bunifu nchini kuwasilisha kazi zao kwa Kamati ya Taifa ya Tuzo hiyo ili kuendeleza juhudi za kukuza uandishi na lugha ya Kiswahili.
“Tumekuwa tukishuhudia mchango mkubwa wa tuzo hii katika kuibua vipaji vipya na kukuza maudhui ya Kiswahili. Ni vyema waandishi wakajitokeza kwa wingi kushiriki,” alisema Prof. Mkenda.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo, Prof. Penina Mlama, alibainisha kuwa miswada itakayopokelewa itahusu nyanja za Riwaya, Ushairi, Hadithi za Watoto na Ushairi kama ilivyokuwa mwaka uliopita. Aliongeza kuwa upokeaji wa miswada utaanza Agosti 15 na kufungwa rasmi Novemba 30, 2025.
“Tunawaalika waandishi wote bunifu kutumia fursa hii ya kipekee kushiriki katika tuzo hii muhimu. Baada ya kupokea miswada, majaji wataanza kupitia kazi hizo na washindi watatangazwa Aprili 13, 2026, siku ya kumbukizi ya kuzaliwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere,” alisema Prof. Mlama.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, aliwashukuru wadau wote wa uandishi bunifu walioshiriki katika kikao cha mazungumzo ya kuboresha tuzo hiyo, akisisitiza kuwa maoni yao yamekuwa chachu ya uboreshaji wa mashindano hayo.
Kikao cha uzinduzi kimehudhuriwa na wadau mbalimbali wa uandishi bunifu ambao walipata nafasi ya kutoa maoni yatakayosaidia kuendeleza na kuinua hadhi ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere.