KOCHA wa Klabu ya Simba, Fadlu Davids, amefunguka kuhusu hali ya kikosi chake, programu ya maandalizi wakiwa kambini nchini Misri, changamoto za usajili na matumaini yake kuelekea msimu mpya wa mashindano ya ndani na kimataifa.
Kupitia mahojiano maalum na mtandao wa klabu hiyo upande wa Youtube, Fadlu ameeleza wanavyoijenga upya Simba, akitumia maandalizi hayo kama msingi wa mafanikio ya baadae.
Akizungumza kwa utulivu, Fadlu anasema: “Kwa sasa tuna makundi mawili ya wachezaji wale waliojiunga nasi wiki iliyopita na wale waliokuja jana. Hii inaleta tofauti katika viwango vya maandalizi, lakini malengo yetu ni kuwafanya wote wafikie kiwango sawa cha kimbinu na kimwili.”
Anasema wachezaji waliowasili mapema walishaanza programu ya mazoezi ya nguvu, wakafanyiwa vipimo vya mwili na tayari wanaelekea kuwa katika hali bora. Wapya bado wanafuata mchakato huo.
“Tunapaswa kuwa makini na wachezaji wapya, hatuwezi kuwapeleka kasi kama wengine. Tunawapima, tunawaandaa, na lengo ni kuwafanya wawe sehemu ya timu inayoelewana ndani ya uwanja,” anasisitiza.
KUONDOKA KWA WACHEZAJI MUHIMU
Kocha huyo mzawa wa Afrika Kusini hajaficha kuwa kuondoka kwa nyota kama Che Malone, Fabrice Ngoma na Mohamed Hussein ni pengo kubwa, lakini halimfanyi ashindwe kupumua.
“Fabrice ni Fabrice, huwezi kumpata mwingine kama yeye lakini unaweza kupata mchezaji mwenye sifa zinazokaribiana. Hilo ndilo tumelifanya kwa usahihi kupitia idara yetu ya utafutaji vipaji,” anasema.
Anampongeza mtaalamu wa usajili, Mels Daalder, kwa kufanikisha usajili wa wachezaji waliolenga kuziba mapengo hayo kwa sifa zinazokidhi mahitaji ya Simba.

Fadlu anafichua kuwa lengo la kambi ya Misri si mazoezi ya kawaida tu, bali ni kujenga msingi wa soka la kisasa wa Simba.
“Tunajenga timu yenye kasi, inayocheza kwa mpangilio wa hali ya juu, inayopresi kwa kasi na kudhibiti mechi kwa kutumia mfumo wa kisasa.”
Anasema wachezaji kama Alassane Kante (kiungo), Semfuko na wengine wameletwa kwa vigezo vya kiufundi na kimfumo, si kwa majina yao.
“Tunajua nini tunahitaji katikati ya uwanja. Tunahitaji wachezaji wanaoweza kucheza pasi fupi na ndefu, wanaoweza kudhibiti nafasi na kucheza kwa akili. Hilo ndilo tunalojaribu kuunda hapa Misri,” anafafanua.

Akizungumzia washambuliaji wapya, Davids amesema Jonathan Sowah ni ‘mnyama wa kufumania nyavu’ ambaye Simba walionja makali yake walipocheza dhidi yake wakati akiwa Singida BS.
“Tayari anaonyesha athari mazoezini, ana njaa, ana nguvu, na anajua kupambana,” anasema.
Kuhusu Morris Abraham, Davids anasema: “Ni kijana mwenye kipaji cha hali ya juu, ana akili ya kiuchezaji, anajua kusoma mchezo kabla ya mpira kumfikia. Na alishafanya kazi nasi kwa miezi miwili iliyopita, hivyo anaelewa mfumo wetu.”

Kwa upande wa Mohamed Bajaber, kiungo aliyewahi kuitwa timu ya taifa ya Kenya, Davids amesema ni mchezaji mwenye akili ya soka la kisasa.
“Ana nidhamu ya hali ya juu, anatunza mwili wake kama mchezaji wa Ulaya. Na ana malengo ya mbali si tu Simba, bali kufika Ulaya,” anasema.
Ameeleza kuwa Bajaber alikumbwa na majeraha madogo, lakini wanafuatilia kwa karibu mchakato wa afya yake na tayari anaonyesha mwanga mzuri.
Davids anasisitiza kuwa kila hatua inayochukuliwa sasa ni ya kiufundi. Wachezaji wanapimwa kwa takwimu, kasi, muda wa mabadiliko ya nafasi, na uwezo wa kuelewa mbinu.
“Tunajenga timu kisayansi. Hii si tu kuhusu kukimbia, ni kuhusu kuelewa mchezo, kuelewana na kushambulia kwa akili,” anasisitiza.
Ameeleza kuwa wachezaji walioko kwenye michuano ya CHAN bado hawajajiunga, lakini anawapongeza kwa hatua waliyoifikia.
“Hawa ni injini ya Simba. Tunawategemea warudi wakiwa tayari. Tunatumaini wataenda mbali zaidi hata fainali,” anasema.
Anasema watakaporudi, hawatakuwa wageni, kwani wanafahamu misingi ya Simba na mbinu zake.

Mwisho, Davids amedokeza kuwa bado kuna wachezaji zaidi wanatarajiwa kujiunga na timu hiyo.
“Kuna majina makubwa yanakuja wapo wa ndani na wa kimataifa. Hatutaki kukurupuka, tunafanya kila kitu kwa mkakati,” anasema.