MWANDISHI wa Habari za Michezo wa Mwanaspoti, Gazeti linalozalishwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd, Nevumba Abubakar ametunukiwa tuzo na Chama cha Mpira wa Miguu kwa Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Arusha (ARAFA) kutokana na kutambua mchango wake katika uandishi wa habari za mchezo huo.
Cheti hicho amekabidhiwa na Mwenyekiti wa ARAFA, Daud Mnongya mapema leo Jumatano, huku mwenyekiti huyo akisema wametambua juhudi za Nevumba wanayemtaja kuwa ni sehemu ya kukua kwa mchezo huo na kutambulika sehemu mbalimbali.
“Juhudi zake za kuunga mkono Mpira wa Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Arusha kupitia vyombo vya habari. Ni wazi kwamba taarifa na habari alizozichapisha kupitia Mwanaspoti zimekuwa zikiwapa ari wachezaji na viongozi wa mpira huu maalum, ambao mara nyingi hupata nafasi ndogo ya kupewa uzito wa kimataifa au kitaifa.” amesema.
“Tunajivunia Mwanaspoti na tutatumia gazeti hili ambalo tunaahidi kulitangaza katika michuano mbalimbali ya ndani na kimataifa kwa kulitaja kuwa ndilo lililokuza mchezo huu kwa kuutangaza tumeamua kumkabidhi cheti Nevumba kwa sababu ndiye kinara katika uandishi wa habari zake.”
Kwa upande wa Nevumba alisema anajisikia fahari kupata heshima hiyo ya kutunukiwa cheti na anaamini huo utakuwa muendelezo wa kuendelea kupambana kuendelea kuukuza mchezo huo kwa kufikisha taarifa kwa jamii kupitia habari.
Cheti hicho kilichotolewa leo Agosti 4 2025, ni cha pili kwa mwandishi huyo baada ya mapema mwaka huu kutunukiwa cheti heshima na Ubalozi wa Marekani, ikiwa ni sehemu ya kutambua umahiri wake katika utengenezaji wa maudhui ya kidigitali.