Stars yaandika rekodi mpya CHAN, ikiizima Mauritania

TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imeandika rekodi mpya katika fainali za CHAN, baada ya kushinda mechi ya pili mfululizo ya Kundi B kwa kuifumua Mauritania kwa bao 1-0 na kufikisha pointi sita.

Stars imepata ushindi huo usiku huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na kuifanya ifikishe pointi hizo ambazo haijawahi kuzipata katika fainali zote ilizowahi kushiriki zikiwamo za CHAN hadi zile za AFCON.

Katika fainali mbili za CHAN za mwaka 2009 na 2020 Stars ilimaliza kwa kuvuna pointi nne tu kwa kila fainali ilizoshiriki, lakini leo iliweza kuvunja mwiko kwa kufikisha pointi sita na kuongoza msimamo wa kundi hilo kwa fainali hizi za nane zinazoandaliwa na nchi za Tanzania, Kenya na Uganda. Pia hata katika fainali tatu za Afcon 1980, 2009 na 2023 Tanzania haikuwahi kufikisha idadi ya pointi hizo sita au kuvuka makundi kwenda mbele, lakini ushindi wa leo umewapa tumaini la kufanya maajabu ikiwa wenyeji.

Bao la beki Shomari Kapombe katika dakika ya 88 yaliipa matumaini Stars ya kuvuka hatua ya makundi kwa mara ya kwanza.

Awali Stars ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso katika mechi ya ufunguzi wa fainali hizo cha CHAN 2024.

Kipindi cha kwanza Mauritania walionyesha upinzani mkubwa wakifunga mianya ya viungo wa Stars kupitisha mipira hasa kwa Feisal Salum ‘Fei  Toto’ na Mudathir Yahya aliyeibuka mchezaji bora wa mechi hiyo.

Dakika 45 za kipindi cha pili, kocha Hemed Suleiman ‘Morocco’ alifanya mabadiliko ya wachezaji wawili alimtoa Yusuph Kagoma baada ya kupewa kadi ya njano na kumuingiza Ahmed Pipino, pia alimuingiza Nassor Saadun na kumtoa Abdul Suleiman ‘Sopu’.

Mabadiliko hayo yalionekana kuwa na manufaa  kwani Kagoma alionekana kutoka mchezoni akiwa mzito kufanya maamuzi na kwa upande wa Saadun baada ya kuingia alishambulia kwa Kasi.

Licha ya kuonekana kulimudu eneo hilo lakini Pipino alishindwa kuendelea baada ya kuumia na nafasi yake ikachukuliwa na Shekhan Khamis dakika ya 72.

Kikosi cha Stars kilichoanza, Yakoub Suleiman, Ibrahim Hamad, Dickson Job, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Idd Seleman, Feisal Salum, Abdul Suleiman ‘Sopu’, Yusuph Kagoma, Mudathir Yahya na Clement Mzize.

kikosi cha Mauritania kilichoanza, Abderrahmane Sarr, Mohamed Ramdane, Demine Saleck, El Mami Tetah, Alassane Diop, Nouh Mohamed, Soukrana M’haimid, El Hacen, Hamady N’diaye, Ahmed Ahmed na Mohamed Said.