Dar es Salaam. Watia nia watatu wa nafasi ya urais kupitia Chama cha ACT Wazalendo, mmoja wa urais wa Zanzibar na wawili wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamejinadi mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho, wakiomba ridhaa ya kupitishwa kuwa wagombea rasmi katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Mkutano huo umefanyika leo Jumatano Agosti 6, 2025 ukiwa na lengo la kuwachuja na kuwapitisha wagombea wa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aliyefungua dimba alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud ambaye ameeleza kuwa anagombea nafasi hiyo kwa nia ya kuendeleza malengo na dira ya chama hicho, pamoja na kuendeleza misingi ya viongozi waliotangulia, akiwamo marehemu Maalim Seif Sharif Hamad.
“Naomba kura zenu ili nipeperushe bendera ya ACT Wazalendo. Nina uzoefu wa kiuongozi katika nyanja mbalimbali, naelewa malengo ya chama chetu na namna ya kuyatekeleza. Kwa unyenyekevu, nawasihi mnipitisha ili tukaikamilishe safari ya viongozi waliotangulia ambao sasa wametangulia mbele ya haki. Hawa wote wanatudai, tuende tukainusuru Zanzibar,” amesema Othman.
Akifuata kwa kuwasilisha sera zake, Aaron Kalikawe ambaye ni mtaalamu wa teknolojia, amesema endapo atapata nafasi hiyo, ataitumia kuinua uchumi wa Tanzania kupitia uwekezaji mkubwa katika sekta ya teknolojia kwa kuvutia kampuni za kimataifa kuwekeza nchini.
“Kila Mtanzania atafaidika kwa kumiliki hisa kwenye kampuni kubwa za kiteknolojia zitakazowekeza nchini. Hii itawawezesha kumiliki majengo ya kisasa kupitia mapato ya hisa hizo,” amesema Kalikawe.
Aidha, ameahidi kuwa kila Mtanzania atakuwa na uhakika wa kupata Sh150,000 kila mwezi bila kikomo, huku kila mwanafunzi wa sekondari akiwa na mwalimu wake binafsi kupitia matumizi ya akili unde (AI).
“Kwa kutumia teknolojia ya akili mnemba, kila Mtanzania atapewa maarifa sawa na ya mtu aliyesoma hadi shahada ya uzamili, bila kujali kiwango chake cha elimu ya awali,” ameongeza Kalikawe.
Mwania wa mwisho aliyewasilisha sera zake ni Luhaga Mpina, ambaye hivi karibuni alijiunga na ACT Wazalendo akitokea CCM.
Mpina amesema anaomba ridhaa ya chama hicho ili kuleta mageuzi makubwa nchini, akisisitiza kuwa, “ACT Wazalendo kutamu sana.”
“Naomba ridhaa yenu ili kutimiza wajibu huu. Dawa ya matatizo tuliyonayo ni Mpina. Nipeni nafasi niende Ikulu kuikomesha rushwa, ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma. Nisimamie Serikali kwa uadilifu,” amesema Mpina.
Mpina, ambaye ni mbunge wa zamani wa Kisesa (Simiyu), alijinasibu kuwa ni mzalendo wa kweli, akitolea mfano mchango wake katika sakata la Tegeta Escrow mwaka 2014 pamoja na Zitto Kabwe na marehemu Deo Filikunjombe.
“Kazi ya kuiondoa CCM madarakani imeiva. Nipeni ridhaa leo ili nikakabiliane na wagombea wa vyama vingine. Mambo kama Katiba Mpya yamekuwa yakipigwa danadana bila sababu, tukimalize huu mchezo,” amehitimisha.