Wanne kortini wakidaiwa kusafirisha kilo 51 za heroin

Dar es Salaam. Ernest Semayoga (48) maarufu Mukri na wenzake watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa kilo 51.47, kinyume cha sheria.

Mbali na Mukri ambaye na mkazi wa Kawe, washtakiwa wengine ni mfanyabiashara Salum Jongo (45) mkazi wa Mbezi Beach; Amin Kesibo (25) mkulima na mkazi wa Mbezi Beach pamoja na Tatu Nassoro (45) mjasiliamali na mkazi wa Veterinary wilaya ya Temeke.

Washtakiwa hao wamefikishwa Mahakamani hapo leo Alhamisi Agosti 7, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 19212 ya mwaka 2025 na wakili wa Serikali, Pancrasia Protas, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga

Hata hivyo, kabla ya kusomewa shtaka lao, hakimu Mwankuga alisema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Vilevile kiasi cha dawa walichoshtakiwa nacho hakina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo watapelekwa rumande.

Baada ya maelezo hayo, Wakili Protas aliwasomea shtaka lao.

Alidai washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Septemba 18, 2020 eneo la Temeke Vetenari jijini Dar es Salaam, walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa kilo 51.47, kinyume cha sheria.

Upande wa mashtaka umedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika hivyo wameomba wapangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuandaa taarifa muhimu kwa ajili ya kuisajili Mahakama Kuu.

Hakimu Mwankuga alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Agosti 20, 2025 kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka linalowakabili halina dhamana.