Dar es Salaam. Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imerekodi ziada ya Dola 0.8 bilioni za Marekani (Sh2.08 trilioni) katika robo ya kwanza ya 2025, kwa mauzo yake ya nje ikilinganishwa na nakisi ya dola bilioni 4.0 (Sh10.4 trilioni) kwa kipindi kama hicho 2024.
Mabadiliko hayo yanahusishwa na ufanisi ulioongezeka wa mauzo ya nje, kuimarika kwa biashara ndani ya Bara la Afrika na ongezeko la ushindani miongoni mwa nchi washirika.
Jarida la takwimu za robo mwaka la EAC kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2025, linaonyesha mauzo ya nje yaliongezeka kwa asilimia 47.3 na kufikia Dola 17.7 bilioni za Marekani (Sh46.02 trilioni).
Pia uagizaji wa bidhaa kutoka nje umeongezeka kwa kiasi kidogo cha asilimia 4.6 hadi Dola 16.8 bilioni (Sh43.68 trilioni).
Jarida hilo linaeleza mauzo ya bidhaa za ndani yalipanda kwa asilimia 48.1, huku mauzo ya bidhaa zilizorejeshwa nje yakiongezeka kwa asilimia 32.4, hali inayoonesha ongezeko la bidhaa zinazozalishwa nchini na zenye thamani ya juu.
Kulingana na jarida hilo, biashara ndani ya bara la Afrika ilichangia kwa kiasi kikubwa katika mafanikio hayo, kwani biashara ndani ya bara ilikua kwa asilimia 53.9 na kufikia dola za Marekani bilioni 9.5, ambayo sasa ni sawa na asilimia 27.5 ya biashara ya EAC.
Biashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pekee, iliongezeka kwa asilimia 53.6 hadi Dola 5.2 bilioni (Sh24.7 trilioni), ikionyesha maendeleo yaliyopatikana kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuondoa vikwazo vya kibiashara.
Takwimu zinaonyesha China imeendelea kuwa mshirika mkubwa zaidi wa kibiashara wa EAC katika robo hiyo ya mwaka, ikifuatiwa na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), India, Afrika Kusini na Japan.
Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha hivi karibuni cha utoaji wa ripoti, ukanda wa EAC ulisajili ziada ya biashara ya Dola 1.8 bilioni za Marekani kwa China.
Hali hiyo imeelezwa kuchangiwa na ongezeko kubwa la mauzo ya bidhaa kwenda kwenye soko la China pamoja na kupungua kwa uagizaji wa bidhaa kutoka nchini humo.
Masoko mengine muhimu ya mauzo ya nje yalijumuisha Afrika Kusini, Hong Kong na Singapore, huku bidhaa zinazoagizwa kwa wingi zikiwa ni bidhaa za mafuta ya petroli, magari, mitambo na plastiki,” jarida hilo linaeleza.
Jarida hilo linaonyesha kuwa shughuli za biashara bado zilijikita katika sekta chache hasa ya mauzo ya bidhaa za metali, madini, kilimo, mawe ya thamani na mitambo kwa pamoja ziliunda zaidi ya nusu ya thamani ya jumla ya biashara ya ukanda huo.
Akizungumzia hali hiyo, Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi, Oscar Mkude amesema ziada ya mauzo nje dhidi ya manunuzi inamaanisha kiasi cha fedha kilichoingia kwenye jumuiya ikilinganishwa ni kilichotoka ni kikubwa.
“Hii ni habari njema lakini sasa tunapaswa kuangalia ukuaji umetoka kwenye maeneo gani na mchango kwa mtu mmoja mmoja au nchi wanachama,” amesema.
Naye Profesa Abe Kinyondo amesema amesema ongezeko la biashara ndani ya ukabda wa EAC ni jambo la kawaida.
“Jambo ambalo tunahitaji kufahamu bidhaa bidhaa nyingi zilizosafirishwa ni ghafi kwasababu hatuongezi thamani bidhaa zetu,hili ni tatizo kwasababu inafanya nchi zetu zinapoteza mapato na ajira nyingi za vijana waliopo mitaani,” amesema.
Kuhusu mfumuko wa bei, jarida hilo linaonyesha mfumuko wa bei kwa mwaka katika ukanda wa EAC, kama unavyopimwa kwa kutumia faharisi ya pamoja ya bei za mlaji (EAC-HCPI), ulifikia asilimia 27.0 mwezi Machi 2025, ukishuka kutoka asilimia 30.6 Februari.
Kwa kulinganisha, kiwango hicho kilikuwa asilimia 6.7 Machi 2024.,mfumuko wa bei wa mwezi hadi mwezi ulikuwa asilimia 0.2 kwa Machi, ikilinganishwa na asilimia hasi 0.5 Februari 2025.
“Wastani wa mfumuko wa bei wa jumla kwa mwaka mzima wa kalenda ya 2024 ulikuwa asilimia 13.5, kutoka asilimia 6.3 mwaka 2023,
“Hili lilichangiwa zaidi na viwango vya juu vya mfumuko wa bei nchini Sudan Kusini na Burundi, vilivyofikia asilimia 99.9 na 20.8 mtawalia,” linaeleza Jarida hilo.
Mfumuko wa bei msingi (ambao haujumuishi bei za chakula na nishati) ulikuwa asilimia 28.9 mwezi Machi 2025, huku mfumuko wa bei wa chakula ukifikia asilimia 49.4 kwa mwezi huo, ukishuka kutoka asilimia 55.6 mwezi Februari 2025.
Mfumuko wa bei wa nishati na huduma za matumizi ya nyumbani uliendelea kuwa thabiti kwa kiasi fulani kwa asilimia 3.3.
Kwa hali ya kifedha, Jarida hilo linaeleza upanuzi wa jumla wa fedha (broad money supply) uliongezeka kwa asilimia 10.1 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, jambo linaloashiria mazingira ya kifedha yaliyojaa ukwasi zaidi katika nchi wanachama.
Ukuaji huu uliungwa mkono kwa kiasi kikubwa na ongezeko la asilimia 21.1 la mikopo halisi kwa serikali, jambo linaloashiria kuendelea kwa upanuzi wa bajeti na ufadhili wa sekta ya umma.
Mikopo kwa sekta binafsi pia iliongezeka kwa asilimia 5.5, ikionyesha urejeo wa taratibu wa shughuli za sekta binafsi.
Vilevile, mali za kigeni halisi (net foreign assets) ziliongezeka kwa asilimia 18.1, zikichangiwa na ongezeko la mapato kutoka nje, yakiwemo marejesho ya fedha kutoka kwa raia wa EAC walioko nje ya nchi.