BAADA ya kukaa nje ya uwanja kwa muda, beki wa zamani wa Biashara United na Singida Fountain Gate, Abdulmajid Mangalo amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia Pamba Jiji.
Awali, beki huyo alikuwa anafanya mazungumzo na Mtibwa Sugar, lakini mambo hayakwenda vizuri sasa ni rasmi ataitumikia Pamba msimu ujao wa 2025-2026 unaoatarajiwa kuanza katikati ya Septemba.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Pamba kimeliambia Mwanaspoti kuwa ni kweli wamemalizana na beki huyo wa kati aliyewahi kuhusishwa na Simba na Yanga katika misimu miwili iliyopita, ambaye wameweka wazi kuwa wamempa mkataba baada ya kujiridhisha kuwa yupo tayari kuipambania timu hiyo.
“Ni kweli hajaonekana uwanjani muda mrefu akiuguza jeraha la goti, taarifa hiyo tunaifahamu na amesaini mkataba baada ya vipimo kuonyesha kuwa tupo fiti na ana uwezo wa kuipambania nembo ya Pamba Jiji,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Ni beki ambaye ukiondoa uzoefu ananidhamu nzuri na ni mpambanaji tunaamini ni chaguo sahihi kwetu ukiangalia tulikuwa na upungufu huo msimu ulioisha kutokana na kuruhusu mabao mengi.”
Alisema usajili wanafanya usajili kwa kuzingatia mahitaji ya kikosi chao.