BAADA ya Singida Black Stars kufikia makubalino na Simba ya kumuachia aliyekuwa nyota wa kikosi hicho, Mghana Jonathan Sowah, mabosi wa timu hiyo wako hatua nzuri ya kumpata mshambuliaji mpya raia wa DR Congo, Malanga Horso Mwaku.
Sowah tangu ajiunge na kikosi hicho dirisha dogo la Januari 2025, akitokea Al-Nasr Benghazi ya Libya, alifunga mabao 13 ya Ligi Kuu Bara, hivyo kuanza kuzivutia klabu mbalimbali za ndani na nje ya nchi zilizokuwa zinaiwinda saini yake.
Sasa baada ya nyota huyo kujiunga na Simba, mabosi wa Singida wanafanya mazungumzo na mshambuliaji, Malanga kwa ajili ya kuongeza nguvu ndani ya kikosi hicho, kwa kushirikiana na washambuliaji wengine waliopo akiwemo pia, Mkenya Elvis Rupia.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza mazungumzo hayo yanaendelea vizuri na kuna mwanga mkubwa wa mchezaji huyo akaichezea Singida msimu ujao, ingawa mabosi wa kikosi hicho wanamuangalia zaidi kwa miaka ya baadaye na si sasa.
“Hatuwezi kusema ni mbadala wa Sowah kwa sababu hana uzoefu wa kutosha, Malanga tunamuangalia zaidi kama mchezaji kijana ila mwenye kipaji kikubwa hivyo, tunaamini ni hazina kwetu mbele kutokana na umri alionao,” kilisema chanzo hicho.
Nyota huyo aliyezaliwa Novemba 12, 2003, ni mmoja wa washambuliaji wanaotabiriwa makubwa kutokana na uwezo alionao, ambapo kwa sasa anacheza FC Saint Eloi Lupopo aliyojiunga akitokea Union Sportive Tshinkunku zote za DRC.