Pemba. Kijana Said Sihaba Khamis (18), amefariki dunia huku wengine wanne wakipotea baada ya mashua kuzama baharini walipokuwa wakisafiri kutoka Muambe kuelekea Unguja kwa shughuli za kibiashara.
Mashua hiyo ilikuwa na jumla ya watu wanane. Taarifa zinaeleza kuwa mmoja amefariki dunia, watatu walijiokoa na wanne hadi sasa bado hawajapatikana.
Mmoja wa walionusurika, Said Hassan Makame (16), mkazi wa Muambe, akizingumza na Mwananchi eneo la tukio leo Alhamisi Agosti 7, 2025, amesema walipoanza kuingia kwenye mkondo wa bahari, mashua yao ilipigwa na dhoruba ikapoteza mwelekea na kuzama. “Wakati tunaingia kwenye mkondo wa bahari, tulikosea njia, mashua ikapigwa na wimbi na kuzama. Nilitumia kifuniko cha ndoo kujinusuru hadi nikafika salama pwani,” amesema Makame.
Naye Abass Makame Khamis, mmoja wa waokoaji amesema walipata taarifa za ajali hiyo jana jioni na walikwenda haraka eneo la tukio, lakini juhudi zao za awali hazikufanikiwa.
Hata hivyo, amesema leo asubuhi walirudi tena wakishirikiana na Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM) na kufanikiwa kuupata mwili wa Said Sihaba Khamis.
“Hali ya bahari haikuwa mbaya sana, lakini tulichelewa kufika eneo la tukio. Hata hivyo, leo tumefanikiwa kuupata mwili wa kijana mmoja,” amesema Abass.

Daktari aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu, Twaha Juma amesema chanzo cha kifo cha kijana huyo ni kushindwa kupumua baada ya kuzama majini.
Mkuu wa Kamandi ya Pemba wa KMKM, Bakari Salum Othman amesema baada ya kupata taarifa ya ajali hiyo jana jioni, alituma kikosi cha uokoaji ambacho kilifanikiwa kuupata mwili wa kijana mmoja.
Amesema bado wanaendelea kuwatafuta vijana wengine wanne ambao hawajulikani walipo.
“Kikosi chetu kitaendelea kushirikiana na wananchi hadi tutakapowapata vijana wote waliopotea,” amesema Othman.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkoani, Miza Hassan Faki amewataka wananchi kuwa na subira katika kipindi hiki, huku akitoa wito wa kuepuka kutumia bandari bubu na badala yake watumie bandari rasmi zilizowekwa na Serikali ili kulinda usalama wa maisha yao.
“Haiwezekani mkaendelea kutumia njia zisizo rasmi wakati Serikali imeweka bandari salama. Hili ni jambo hatari kwa maisha yenu,” amesema Miza.