Chadema yavuka kizingiti cha kwanza kupinga amri za zuio

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimevuka kizingiti cha kwanza cha pingamizi la awali katika shauri la maombi ya marejeo dhidi ya amri za zuio la kufanya siasa na kutumia mali za chama hicho.

Juni 10, 2025, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam ilitoa amri za zuio la kufanya shughuli za kisiasa kwa Chadema na kutumia mali zake.

Mahakama ilitoa amri hizo kusubiri kuamuliwa kwa kesi ya Kikatiba inayokikabili chama hicho kuhusu mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali za chama hicho.

Amri hizo zilitolewa na Jaji Hamidu Mwanga anayesikiliza kesi hiyo kutokana na shauri la maombi ya zuio la muda lililofunguliwa na walalamikaji katika kesi ya msingi.

Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 imefunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema-Zanzibar, na wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.

Walalamikiwa ni Bodi ya Wadhamini waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.

Sambamba na kesi hiyo, walalamikaji walifungua shauri dogo la maombi ya zuio la muda dhidi ya wadaiwa, wakiiomba Mahakama itoe amri ya kuwazuia kufanya shughuli zozote za kisiasa na kutumia mali za chama mpaka kesi hiyo ya msingi itakapoamuliwa.

Walalamikiwa waliwasilisha pingamizi la awali dhidi ya kesi ya msingi na shauri dogo la maombi ya zuio.

Juni 10, 2025, Mahakama iliyatupilia mbali yote, kisha ikasikiliza shauri la maombi ya zuio na katika uamuzi wake, ilikubaliana na hoja za walalamikaji.

Hivyo, ilitoa amri ya zuio kwa walalamikiwa kujishughulisha na shughuli zozote za kisiasa, na pia ikawazuia wao binafsi, wakala wao au mtu yeyote anayefanya kazi kwa maelekezo au kwa niaba yao, kutumia mali za chama hicho mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.

Hata hivyo, walalamikiwa hawakuridhika na uamuzi huo, hivyo wakafungua shauri la marejeo wakiiomba Mahakama irejee na kisha iondoe amri hizo, wakidai zilitolewa isivyo halali.

Shauri hilo namba 14982/2025, kabla ya kuanza kusikilizwa, walalamikaji katika kesi ya msingi wameibua pingamizi la awali wakiiomba Mahakama ilitupilie mbali shauri hilo bila kulisikiliza, wakibainisha sababu mbili.

Hata hivyo, Jaji Mwanga katika uamuzi baada ya kusikiliza hoja za pande zote kuhusu pingamizi hilo, amelikataa na kuamua kuendelea na usikilizwaji wa shauri la marejeo.

Sababu ya kwanza, Wakili Alvan Fidelis amedai inahusu uhalali wa Mahakama kusikiliza maombi hayo.

Amedai aya ya 11, 13(d), (g) na aya ya 14 zinabeba sababu za marejeo, ingawa walichoomba katika hati ya madai ni kutengua amri za zuio la muda za Juni 10, 2025.

Amedai sababu hizo zilizotolewa zinahusu haki ya kutokusikilizwa, yaani kwa kutokupewa haki ya uwakilishi.

Wakili huyo amedai maombi hayo yameomba kutengua amri za zuio, lakini pia yameletwa kama mbadala wa mapitio.

Fidelis amedai hata kama wangetoa sababu sahihi za marejeo, bado maombi hayo yasingekuwa halali kwa sababu amri wanazoomba kuzitengua ni amri zisizomaliza shauri kwani haziamui haki za wadaawa.

Wakili Fidelis ameirejesha Mahakama katika uamuzi wa kesi mbalimbali zilizoamuliwa na Mahakama hiyo katika kujenga hoja.

“Kwa mazingira hayo tunaomba pingamizi letu likubaliwe na maombi yao yawe dismissed (yafutwe),” ameomba.

Akijibu hoja hiyo, wakili wa walalamikiwa, Jeremiah Mtobesya amesema pingamizi hilo halina mashiko kwa kuwa mamlaka ya Mahakama kusikiliza shauri ni suala la kisheria na si la kudhani.

Amedai hati ya maombi ya shauri hilo, ambayo ndiyo inabeba maombi anayoyaomba, pia inaonesha mamlaka ya Mahakama kusikiliza shauri hilo.

Mtobesya amebainisha kuwa maombi hayo yamefunguliwa chini ya Amri ya 7, Kanuni ya 5, ambayo inaeleza mtu ambaye hajaridhika na amri ya zuio anaweza kufungua maombi ya marejeo mahakamani.

“Tulichokileta katika maombi yetu kwanza, tunaomba kutengua amri za Juni 10, 2025,” amesema, huku akisisitiza kuwa kwa kifungu hicho, Mahakama hiyo ina mamlaka ya kisikiliza maombi hayo.

Kuhusu mambo yaliyotajwa kwenye aya za kiapo kama zina mashiko au la, amedai mawakili wa walalamikaji walipaswa kusubiri mpaka usikilizwaji wa shauri hilo kwanza, ndipo waone kama zina mashiko au la.

Mtobesya amedai kama wana shida na aya fulani kwenye kiapo, wanapaswa kubainisha aya zinazoweza kuondolewa kwenye kiapo kama Mahakama inaridhika nazo.

“Kwa sababu hiyo pingamizi lao halina mashiko,” amedai.

Hoja kwamba wangeweza kufungua shauri la mapitio, amesisitiza walichowasilisha mahakamani ni maombi ya marejeo.

Akijibu hoja ya kufutwa shauri hilo ambalo halijasikilizwa, amesema nafuu yake ni kulitupilia mbali na si kulifuta.

“Kwa kusema hayo, tunaomba pingamizi lao litupiliwe mbali tuendelee na usikilizwaji wa maombi,” ameomba Mtobesya.

Wakili Rugemeleza Nshala amesisitiza kuwa sheria inatoa nafasi kwa mtu ambaye hajaridhika na amri zilizotolewa kurudi katika Mahakama hiyohiyo kuomba zifutwe.

Amedai mawakili wa walalamikaji hawajasema kuwa kile ambacho wanaomba kitenguliwe si ambacho kilitolewa na Mahakama.

Hoja kwamba amri zinazoombwa kufutwa hazikatiwi rufaa, amesisitiza kuwa sheria iko wazi, ambaye hajaridhika anaweza kurudi katika Mahakama husika.

Hivyo, ameiomba Mahakama ilitupilie mbali pingamizi hilo kwa gharama (walipwe gharama za usikilizwaji wa shauri hilo).

Wakili Fidelis amepinga hoja hizo akidai pengine wakati anatoa hoja zake hawakumsikiliza vizuri.

Amedai hajashughulika na hati ya maombi bali kiapo, ambapo amedai wanaomba rufaa kwa mlango wa nyuma kwa kutumia hoja za uhalali wa amri ambazo ni sababu za mapitio.

Amepinga kuwa kama kuna suala la mamlaka ya Mahakama hawapaswi kusubiria mpaka shauri lisikilizwe.

“Kwa mazingira hayo tunaomba shauri hili litupiliwe mbali kwa gharama,” ameomba.

Jaji Mwanga baada ya kusikiliza hoja za pande zote amekataa pingamizi hilo, akisema Mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza na kubadili amri zake.

“Kwa hiyo ninalikataa pingamizi hili ili twende kwenye usikilizwaji wa maombi,” amesema.

Baada ya uamuzi huo, Jaji Mwanga ameendelea na usikilizaji wa shauri hilo.

Katika kesi ya msingi, walalamikaji wanadai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za Chadema na rasilimali za kifedha kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume cha Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.

Pia wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga Muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.