Dar es Salaam. Awamu ya kwanza ya mabasi yaendayo haraka yatakayotoa huduma katika awamu ya pili ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) yamewasili nchini, huku baadhi ya miundombinu ikiwa haijakamilika na mingine ikianza kuharibika.
Mabasi hayo 99 ya Kampuni ya Mtanzania, Mofat, ni sehemu ya yale 250 yatakayotoa huduma katika njia hiyo, huku mengine yakitarajiwa kuwasili mwisho wa Agosti mwaka huu, tayari kuwahudumia Watanzania.
Mabasi hayo yamewasili kutoka China yalikotengenezwa, na taarifa ambazo Mwananchi limedokezwa ni kwamba yamewasili tangu Agosti 5, 2025, na kuanza kupakuliwa kutoka melini katika Bandari ya Dar es Salaam.

Njia yatakayotoa huduma mabasi hayo, inahusisha barabara ya Mbagala hadi Gerezani yenye urefu wa kilomita 20.3, iliyojengwa na Kampuni ya Sinohydro kutoka China, na ilikabidhiwa kwa DART tangu Agosti 2023.
Katika awamu hiyo, kampuni ya Mofat ndiyo imepewa mkataba wa miaka 12 kutoa huduma hiyo, na mabasi yake yatatumia nishati ya gesi asilia.
Kutokana na hatua hiyo yenye matumaini kwa wakazi wa Mbagala na wanaotumia njia hiyo, Mwananchi leo Agosti 7, 2025, ilitembelea miundombinu yatakapopita mabasi hayo kujionea hali halisi. Baadhi ya maeneo yalikutwa hayajakamilika yakiendelea na ujenzi na mengine kuharibiwa.
Maeneo ambayo ujenzi wake umeonekana kuendelea ni kipande cha barabara ya mabasi hayo maeneo ya Kamata, Kariakoo, ambako walishuhudiwa mafundi wakiendelea na kazi.

Pia, miundombinu mingine ambayo bado haijakamilika ni ya mageti janja kwa ajili ya abiria kuingia ndani ya vituo kwa kutumia kadi na siyo tiketi.
Katika hili, Mwananchi imepita katika vituo hivyo kuanzia Kamata hadi Mbagala Rangi Tatu, hakuna hata kimoja ambacho tayari kimefungwa mageti hayo.
Aidha, katika uharibifu wa miundombinu, baadhi ya taa za kuongozea magari zimeharibika na nyingine nguzo zake kuanguka.
Pia, taa nyingine zimevunjwa, jambo linalochangiwa na kupita kwa magari ya mizigo kutoka bandarini.
Wakati hali ikiwa hivyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), Dk Athuman Kihamia, amekiri miundombinu hiyo kutokamilika na kueleza kuwa kwa eneo la Kamata, mabasi hayo yatapita yanapopita magari mengine kwa sasa mpaka hapo ujenzi utakapokamilika.
“Kutokamilika kwa kipande kile hakuna athari kwa kuwa ni padogo tu, hivyo na hayo mabasi yatapita kunapopita magari mengine kwa sasa. Si umeona licha ya ujenzi huo kuendelea, gari zinapita kama kawaida, basi na yenyewe yatapita humo humo,” amesema Dk Kihamia.

Kuhusu kutofungwa kwa mageti janja, amesema kazi hiyo inatarajiwa kuanza mwezi ujao na kwa sasa kitakachofanyika ni abiria kutumia tiketi kwa muda wa mpito.
“Ni kweli mageti janja bado hayajafungwa. Tunategemea kazi hiyo itaanza mwezi ujao, lakini hii haiwezi kuwa sababu mabasi hayo kutoanza kutoa huduma, kwani tumeona abiria waanze kutumia tiketi kwa kipindi cha mpito,” amesema mtendaji huyo.
Kuhusu gesi, amesema kuna kituo cha kujazia ndani ya kituo kikubwa cha mabasi hayo cha Mbagala, hivyo suala la gesi halitasumbua.
Alipoulizwa ni lini hasa mabasi hayo yataanza kazi, amesema lengo ni ndani ya mwezi huu kwa kuwa bado hayajamaliza kupakuliwa bandarini, hivyo ni vigumu kuahidi.
“Unajua licha ya kazi ya kuyapakua kwenye meli mabasi hayo kuanza tangu juzi, kazi hiyo inaendelea hadi ninavyozungumza na wewe hapa, na tumelazimika kuyaombea kibali cha dharura kwa kuwa wananchi wameshayasubiria sana.
“Hivyo kazi hii itakapokamilika ni matumaini yetu kabla ya mwezi huu haujaisha basi yawe yameanza kutoa huduma barabarani,” amesema Dk Kihamia.
Kuhusu madereva waliokidhi vigezo vya kuendesha, amesema wapo 150 tayari kuingia barabarani na kazi hiyo ya kuwasaili iliachwa Mamlaka ya Usafiri Ardhini (LATRA), Jeshi la Polisi wa Usalama Barabarani na Chuo cha Usafirishaji (NIT).
“Kufika kwa mabasi ni jambo moja, lakini kuanza kutoa huduma ni jambo jingine, kwani hii siyo mara ya kwanza kuahidiwa. Labda tutaamini pale tutakapoyaona barabarani,” amesema Shabani Juma.

Ally Biasi amesema magari hayo yakianza kazi wananchi wataweza kutoka na kurudi majumbani kwao kwa wakati, huku akiwataka wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha abiria wanapata usafiri huo kwa muda na si kukaa muda mrefu vituoni.
Kwa upande wa Kasiro Anania, amesema ujio wa mwendokasi ni salama kwa wananchi kwa kuwa wengi kutokana na tabu ya usafiri wamejikuta wakipanda bodaboda, ambayo wakati mwingine badala ya kukuharakisha kwenye shughuli zako, inakuharakisha kwenye kifo.
Zainabu Ayoub, mkazi wa Mbagala Zakhem, ameomba pamoja na yote, waendeshaji wa mabasi hayo kuwawekea utaratibu mzuri wanafunzi, hata wa kuwa na mabasi yao, kwani wamekuwa wakinyanyasika katika usafiri na wakati mwingine wazazi inawaumiza lakini hawana namna.
“Ikiwezekana kwenye suala la wanafunzi, watuambie hata wazazi tuchangie Sh300, lakini watoto wetu wawe na uhakika wa usafiri bila kubughudhiwa. Kuliko ilivyo sasa, wamekuwa wakinyanyasika sana,” amesema Zainabu.
Abbas Kaniki, mkazi wa Chamazi, ameshauri kuwepo na unafuu wa nauli, kwa kuwa hakuna asiyejua kuwa wakazi wa ukanda huo wengi ni wale wanaoishi maisha ya kipato cha chini.
“Huku Mbagala wengi wetu maisha yetu ni ya chini. Serikali inaweza hata kutufanyia nauli Sh500, kwa kuwa tunajua hii siyo biashara bali ni huduma ya umma. Yenyewe itajua itajaziaje huko kwa mwekezaji, na kwa kufanya hivyo ndiyo italeta maana nzima ya maisha bora kwa kila Mtanzania,” amesema Kaniki.