KENYA imenusurika kupoteza mechi ya kwanza nyumbani ikilazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Angola kwenye mchezo wa pili wa Kundi B wa Fainali za Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).
Mchezo huo ambao umepigwa Uwanja wa Moi Kasarani jijini Nairobi umeshuhudia Angola wakiwa wa kwanza kupata bao mfungaji akiwa Joaquim Christovao Paciencia katika dakika ya saba.
Hata hivyo, wenyeji wamefanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 12 kwa mkwaju wa penalti mfungaji akiwa mshambuliaji Austin Odhiambo likiwa ni bao lake la pili kwenye fainali hizo.
Penalti hiyo ilitokana na mshambuliaji huyo wa Gor Mahia kuchezewa vibaya wakati anajaribu kufunga.
Kenya imelazimika kucheza pungufu kwa zaidi ya dakika 70 baada ya kiungo wake Marvin Nabwire kuonyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja
Nabwire alikutana na kadi hiyo nyekundu baada ya kumchezea vibaya mchezaji wa Angola wakati akiwa mchezaji wa mwisho ambapo uamuzi kupitia msaada wa VAR ulimnasa kiungo huyo na kufutiwa kadi ya njano aliyopewa awali na kuwa nyekundu ya moja kwa moja.
Kenya licha ya kucheza pungufu pongezi kubwa zitakwenda kwa safu ya ulinzi iliyozima mashambulizi mengi ya Angola.
Wakati mchezo huo ukielekea mwisho dakika ya 90+5 Angola ilipata bao ambalo liliuzima karibu uwanja mzima wa mashabiki zaidi ya 45,000, lakini baada ya marudio ya VAR ilibainika Paciencia alikuwa ameotea.
Uamuzi huo uliwaibua mashabiki wa Kenya kwa furaha huku Angola wakiumizwa na kufanya mchezo huo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Matokeo hayo yanaifanya Kenya kusalia kileleni mwa msimamo wa Kundi A wakijikusanyia pointi nne baada ya kushinda mechi ya kwanza na sare ya leo, huku Morocco ikiwa nafasi ya pili na pointi tatu sawa na DR Congo wakati Angola ikibaki nafasi ya tatu ikiwa na alama moja na Zambia ikishika mkia bila alama yoyote.